Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Wananchi wa Mtaa wa Chinyoyo, Kata ya Kilimani Jijini Dodoma wako katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu kutokana na taka kuachwa muda mrefu bila kuondolewa na kampuni ya usafi wa mazingira.
Taka hizo zimeripotiwa kukaa kwa zaidi ya miezi miwili na nusu katika maeneo mbalimbali ya mtaa huo, hali inayosababisha uchafu kuzagaa na kuongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa, hususan kwa watoto wanaocheza karibu na maeneo hayo.
Wananchi wamesema hali hiyo imekuwa kero kubwa licha ya wao kulipia huduma ya ukusanyaji taka, huku wakitaka hatua za haraka zichukuliwe ili kulinda afya za jamii.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Chinyoyo, Mhe. Faustina Bendera, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema tayari amewasiliana na kampuni husika pamoja na TARURA kutokana na ubovu wa barabara unaochangia magari kushindwa kufika.
Amesema juhudi zinaendelea kuhakikisha miundombinu inaboreshwa ili kuruhusu huduma ya usafi kufanyika kwa ufanisi, huku akiwataka wananchi kuchukua tahadhari na kuweka taka sehemu rasmi zinazofikika kwa urahisi.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro, amesema kampuni ya usafi imeelekezwa kuchukua hatua za haraka kuondoa taka hizo, akisisitiza kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la pamoja kati ya serikali na wananchi.


Social Plugin