Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UVCCM BUKOBA YATOA VIFAA VYA MICHEZO KUELEKEA MASHINDANO YA “BUKOBA CUP 2026”


Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM Bukoba Bw. James MichaelNyamanza (kulia) akimkabidhi zawadi za washindi wa mashindano ya UVCCM BUKOBA CUP 2026 Katibu wa Chama cha Mpira Wilaya ya Bukoba Bw. Mwinyi Mohamed Mwinyi (kushoto) na katikati ni Katibu wa chama cha mpira Mkoa wa Kagera Bw. Ali Amini Abdul

**

Na Mbuke Shilagi Kagera. 

Mwenyekiti wa UVCCM Manispaa ya Bukoba, James Michael Nyamanza, amekabidhi jezi na mipira kwa wawakilishi wa Kata zote 14 za manispaa hiyo ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya UVCCM Bukoba Cup 2026 yanayotarajiwa kuanza rasmi Ijumaa, tarehe 24 Aprili 2026.

Katika hafla hiyo, mwenyekiti huyo pia amekabidhi zawadi zitakazotolewa kwa washindi kwa Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Bukoba, akisisitiza kuwa lengo la mashindano hayo ni kuwakutanisha vijana, kujenga mahusiano, kuibua na kuendeleza vipaji pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia michezo.

Ameeleza kuwa kupitia mashindano hayo, vijana watapata fursa ya kuonesha uwezo wao huku wakijenga nidhamu na mshikamano, mambo ambayo ni muhimu katika maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Bukoba, Mwinyi Mohamed Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa kufuata taratibu zote za michezo, akieleza kuwa shughuli yoyote ya michezo katika ngazi ya wilaya lazima ipitie kwa viongozi husika na kupata kibali kinachotolewa hadi ngazi ya Mkoa kwa kuzingatia kanuni na sheria za michezo.

Amefafanua kuwa mashindano hayo yataendeshwa kwa kuzingatia Sheria 17 za mpira wa miguu, huku kila Kata ikicheza mechi za nyumbani na ugenini, pamoja na kuzingatia mfumo wa bao la ugenini.

Naye Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera, Ali Amin Abdul, amempongeza Mwenyekiti wa UVCCM Bukoba kwa kuanzisha mashindano hayo pamoja na kudhamini vifaa na zawadi kwa washindi. 

Huku akibainisha kuwa kuanzia hatua ya robo fainali na nusu fainali, mechi zitachezwa kwa dakika 90 na endapo sare itatokea, mshindi atapatikana kwa njia ya mikwaju ya penalti, huku fainali ikichezwa kwa dakika 90 pamoja na dakika 30 za nyongeza kabla ya penalti iwapo sare itaendelea.

Ikumbukwe kuwa, mashindano ya UVCCM Bukoba Cup 2026 yanatarajiwa kuanza rasmi Ijumaa, tarehe 24 Aprili 2026, ambapo mchezo wa ufunguzi utazikutanisha timu za Kashai na Bilele katika Uwanja wa Kaitaba stadium.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com