Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM YAMVAA HECHE, YAIBUA SIRI YA MIKAKATI WA KUOKOA UCHUMI





Na Dotto Kwilasa,DODOMA

Wakati mjadala wa kisiasa ukichukua sura mpya kufuatia kauli za Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na msimamo mzito kikimtaka kuacha upotoshaji huku kikitoa mwongozo wa kimkakati wa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta nchini.

CCM kupitia Katibu wake wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, kimesema ni muhimu mjadala wa kitaifa ukajengwa katika msingi wa ukweli na uwajibikaji badala ya kauli zinazoweza kupotosha umma.

Akizungumza leo Aprili 7,2026 Jijini Dodoma, Kihongosi amemkosoa Heche akimtaka kuacha kauli za upotoshaji na badala yake kuzungumza kwa uhalisia, akieleza kuwa Serikali iliyopo ni sikivu na inaendelea kuchukua hatua kukabiliana na changamoto zilizopo.

Amegusia pia suala la uhuru wa maoni, akibainisha kuwa uhuru huo haupaswi kuchanganywa na matusi au kauli za kudhalilisha, bali unapaswa kutumika kwa staha, ukweli na kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.

Pamoja na mjadala huo, chama hicho kimetoa maagizo matano mahsusi kwa Serikali yenye lengo la kupunguza makali ya ongezeko la bei ya mafuta na kulinda ustawi wa wananchi pamoja na uchumi wa Taifa.

Ametaja miongoni mwa hatua hizo ni kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kuhimili mabadiliko ya bei za mafuta ambao uko katika hatua za mwisho za maandalizi, hatua itakayosaidia kudhibiti misukosuko ya soko la nishati.

Aidha, ameielekeza Serikali kuendelea kuimarisha hifadhi ya mafuta ya kimkakati ili kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa wa uhakika wakati wote, sambamba na kuwekeza katika miundombinu ya kuhifadhi mafuta ikiwemo kituo kikubwa cha Kigamboni.

Kwa mujibu wa CCM, hatua hiyo itapunguza gharama za uingizaji na usambazaji wa mafuta nchini na hivyo kupunguza mzigo kwa wananchi.

Katika kuongeza ufanisi, chama hicho pia kimependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa pamoja wa upokeaji mafuta katika ghala moja, lengo likiwa ni kuondoa ucheleweshaji pamoja na kudhibiti udanganyifu unaoweza kujitokeza katika mchakato wa uingizaji.

Sambamba na hilo, CCM imeitaka Serikali kuimarisha uwezo wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ili liweze kununua mafuta moja kwa moja bila kupitia kwa madalali, hatua itakayosaidia kupunguza gharama zisizo za lazima.

Kihongosi pia amesisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika usafiri wa umma pamoja na matumizi ya nishati mbadala kama gesi asilia, hususan kwa magari ya Serikali, bodaboda na bajaji ili kupunguza utegemezi wa mafuta.

Alieleza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta ni changamoto ya kimataifa inayochangiwa na mabadiliko ya soko la dunia pamoja na migogoro ya kisiasa ikiwemo vita ya Urusi na Ukraine na mivutano ya Mashariki ya Kati.

Ameongeza kuwa Serikali imewahi kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 100 mwaka 2022 ili kupunguza makali ya hali hiyo, akibainisha kuwa hatua kama hizo zinaweza kuendelea kadri itakavyohitajika.

“CCM inaamini Serikali itaendelea kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu huku ikiangalia uwezekano wa kutoa ruzuku pale inapobidi,” amesema Kihongosi.

Pia chama hicho kimewataka Watanzania kuendelea kuwa watulivu na kuepuka upotoshaji unaoweza kuleta taharuki, kikisisitiza kuwa mshikamano na amani ni msingi wa maendeleo ya Taifa.

CCM imehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa mijadala ya kitaifa kufanyika kwa heshima na uwajibikaji, huku ikiendelea kuhimiza ushirikiano kati ya wananchi na Serikali katika kulinda uchumi wa nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com