Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DARAJA HALIBAGUI: MLOLWA ATOA WITO WA AMANI, CHEREHANI NA WANANCHI WASHUKURU KUONDOKA KERO YA MASIKA


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amesisitiza umuhimu wa kulinda amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, akieleza kuwa mafanikio ya miradi ya maendeleo yanategemea sana uwepo wa utulivu wa nchi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Aprili 13,2026 katika Kijiji cha Mwabomba, Kata ya Idahina, Jimbo la Ushetu, Mlolwa alieleza kuwa maendeleo yanayoonekana ni matokeo ya utekelezaji wa ahadi na Ilani ya CCM, huku akitumia Daraja la Mwabomba kama mfano hai.

“Daraja halibagui, uwe mwana CCM, uwe Mwanasiasa wa chama kingine, uwe rangi yako ikoje wewe pita tu, au unafikiri Samia Suluhu Hassan atapita yeye tu pale. Tuachane na hawa wanaobeza tu kila kitu, kila wakati. Wakati wa kampeni tulisema lazima tutengeneze miundombinu ya barabara, tuwaletee maji, umeme, huduma za afya,” amesema Mlolwa.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wananchi kuendelea kuwaunga mkono viongozi waliopo madarakani ili kudumisha mwelekeo wa maendeleo na kulinda amani ya nchi.
“Endeeleni kumuunga mkono mbunge, endeleeni kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan. Msidanganywe na mtu yoyote, Chama Cha Mapinduzi na serikali yake, tunataka utulivu, amani ya nchi yetu imeletwa na serikali inayoongozwa na Dkt. Samia na sera za CCM,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mlolwa amesisitiza wajibu wa wananchi kulinda miundombinu iliyojengwa kwa gharama kubwa za serikali, akieleza kuwa daraja hilo ni mradi wa kihistoria uliomaliza changamoto ya muda mrefu.

“Tunampongeza Mhe. Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili. Watanzania walikuwa wanapoteza maisha kwa sababu ya daraja la zamani. Hili ni jambo la kihistoria, eneo hili lilikuwa na changamoto kubwa hasa kipindi cha maji mengi,” amesema.

“Hili ni daraja la kiwango kikubwa linalorahisisha usafiri kwenda Urambo, Kaliua hadi Geita. Ni lazima tulilinde kwa nguvu zote. Nawapongeza pia Mbunge na wananchi kwa kusimamia maendeleo haya,” ameongeza Mlolwa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, amesema Daraja la Mwabomba limeondoa kero iliyokuwa ikiwasumbua wananchi kwa muda mrefu, hasa wakati wa masika.
“Daraja lilikuwa kero na maumivu makubwa kwa wananchi wa Masumbwe na Mwabomba. Kipindi cha masika watu walikuwa wanateseka sana, wengine walishindwa kuvuka na hata kuhatarisha maisha yao. Leo tunashukuru daraja hili limekamilika na wananchi wanapita bila shida,” amesema Cherehani.

Amebainisha kuwa ujenzi wa daraja hilo lenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 umefikia asilimia 99, huku kazi zilizobaki zikiwa ni hatua ndogo ndogo za mwisho.

“Mradi wa Mwabomba umefikia asilimia 99, kilichobakia ni kazi ndogo ndogo kama kuweka alama. Mkandarasi anaendelea na hatua za mwisho na hatuna madai naye. Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kutupatia fedha hizi,” amesema.

Nao wananchi wa Mwabomba wameeleza kufurahishwa na kukamilika kwa daraja hilo, wakisema limeleta nafuu kubwa hasa wakati wa mvua.
Mkazi wa Mwabomba, Juma Mwendesha Nigula, amesema:
 “Kipindi cha masika daraja la mwanzo lilikuwa linafunikwa na maji mengi, hali iliyokuwa ikitutesa sana. Leo tunatoa shukrani kwa mbunge na Rais kwa kuendelea kutatua changamoto za wananchi. Sasa tunavuka bila hofu.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com