Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZAIDI YA MADHABAHU: KANISA LASHIRIKI KUZALISHA UMEME WA GRIDI YA TAIFA MAKETE




Katika kile kinachoonekana ni mapinduzi ya fikra na ushiriki wa taasisi za dini kwenye maendeleo ya kimkakati, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini, limevuka mipaka ya huduma za kiroho na kuanza kuzalisha nishati ya umeme.

Kupitia mradi wa kufua umeme wa Ijangala wilayani Makete, kanisa sasa linachangia maendeleo ya taifa kwa kuingiza kilowati 360 moja kwa moja kwenye Gridi ya Taifa.

Hatua hiyo ni kielelezo cha ujakonia wa vitendo, ambapo kanisa linashirikiana bega kwa bega na Serikali kupitia Wakala ya Nishati Vijijini (REA) kutatua kero ya nishati, huku mradi huo ukigharimu kiasi cha Shilingi bilioni 2.6.

Mradi huu uliopo katika Kijiji cha Masisiwe, umewezeshwa kwa kiasi kikubwa na ufadhili wa REA, ambapo Shilingi bilioni 1.63 zilitolewa kama ruzuku na Shilingi milioni 922 kama mkopo wa muda mrefu.

Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi wa REA, Emmanuel Yesaya, anabainisha kuwa ushirikiano huo ulianza tangu hatua za awali za andiko la mradi na upembuzi yakinifu, lengo likiwa ni kuhakikisha taasisi zisizo za kiserikali zinashiriki kikamilifu katika uzalishaji wa nishati safi.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Jinsia wa Dayosisi hiyo, Sylvia Sanga, ameeleza kuwa kiu ya maendeleo ndiyo iliyozaa mradi huo. Baada ya kukabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji wa miradi yao ya kijamii, ikiwemo kiwanda cha ushonaji, kanisa liliamua kutumia rasilimali ya maji iliyopo eneo hilo kuanzisha mradi huu ambao sasa umekamilika na kuanza kuliuzia umeme Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Kukamilika kwa mradi huu Machi mwaka huu, hakuleti tu mwanga katika Wilaya ya Makete, bali kunasaidia kutuliza changamoto ya upungufu wa umeme mkoani Njombe kwa ujumla. Ni hatua inayoungwa mkono na falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kushirikisha sekta binafsi na taasisi za kijamii katika kuimarisha miundombinu ya nchi.

Kama anavyosema Meneja wa mtambo huo, Daudi Sanga, huu ni wakati wa taasisi za dini kuona fursa za maendeleo na kuzichangamkia kwa faida ya waumini na taifa kwa ujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com