Katika kile kinachoonekana kuwa ni mkakati wa makusudi wa kutoa elimu ya kina kuhusu uwekezaji nchini, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ametoa ufafanuzi mzito unaolenga kukata mzizi wa fitina kuhusu mjadala wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la Nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Profesa Kitila amebainisha kuwa madai yanayoenezwa kuwa bandari imeuzwa hayana mashiko yoyote ya kisheria wala kiuchumi, kwani hakuna serikali yoyote duniani yenye mamlaka ya kuuza mali ya asili na ya kimkakati kama bandari.
Waziri amefafanua kuwa mjadala mkubwa ulioibuka mwaka 2023 ulitokana na baadhi ya wananchi kutofahamu mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa miradi ya maendeleo, hususan mfumo wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Alieleza kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) haijauza rasilimali hiyo, bali imetoa kandarasi za uendeshaji kwa kampuni za DP World na ADANI ili kuleta ufanisi ambao ulikuwa ukikosekana kwa muda mrefu. Katika mfumo huu, serikali inabaki kuwa mmiliki wa ardhi na miundombinu, huku mbia binafsi akileta teknolojia, mitaji, na uzoefu wa kimataifa katika utendaji wa kila siku.
Matokeo ya uwekezaji huo tayari yameanza kuonekana kwa kasi kubwa, ambapo ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka kwa kiwango ambacho Waziri amekiita ni cha kihistoria.
Ripoti zinaonyesha kuwa meli nyingi sasa zinahamia Tanzania kutoka bandari za nchi jirani kutokana na kasi ya upakuaji mizigo na kupungua kwa muda wa meli kusubiri nangani. Hali hii inathibitisha kuwa uamuzi wa serikali kutoa fursa kwa makampuni yenye uzoefu duniani kufanya kazi kando ya TPA umekuwa na tija kubwa kwa uchumi wa taifa na mapato ya serikali.
Pamoja na mafanikio hayo ya bandarini, Profesa Kitila amebainisha kuwa serikali inaendelea na mapinduzi makubwa ya kiuchumi kupitia mfumo wa PPP, ambapo miradi 101 tayari imeibuliwa katika sekta mbalimbali.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, miradi hiyo imefanyiwa kazi katika hatua tofauti, kuanzia hatua za mawazo ya miradi, upembuzi yakinifu, hadi kufikia utekelezaji kamili. Hii ni ishara kuwa serikali imejipanga kutumia mitaji ya sekta binafsi kuchochea maendeleo ya miundombinu na huduma za kijamii bila kuongeza mzigo wa madeni kwa taifa au kupoteza umiliki wa mali za umma.
Mkakati huu wa PPP ni sehemu ya maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2026 hadi 2031, ukilenga kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kitovu cha uwekezaji na biashara katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Kwa kuwapa nafasi wawekezaji kama DP World na ADANI, serikali inajenga mazingira ya ufanisi ambayo yatadumu kwa muda mrefu, huku ikihakikisha kuwa rasilimali za taifa zinalindwa kisheria na kubaki chini ya udhibiti wa mamlaka za ndani kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Social Plugin