
Siku ya Jumatano, Machi 11, 2026, imeweka alama ya mabadiliko makubwa katika mfumo wa utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita. Badala ya taarifa za kawaida za itifaki, Serikali imetangaza kuwa sasa kipimo cha 'kubaki ofisini' kwa wakuu wa mikoa na wakurugenzi nchini kitakuwa ni idadi ya wawekezaji wapya na ukuaji wa biashara kwenye maeneo yao.
Kwa kauli hiyo maana yake huu sio tena msimu wa 'mazoea,' ni msimu wa matokeo.
Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba amebadilisha kanuni za mchezo na kuanzia sasa, kila Mkuu wa Mkoa anaposimama mbele ya viongozi wa kitaifa, hatatoa tena taarifa za jumla za utawala, bali atawasilisha 'Hati ya Matokeo ya Uwekezaji.' Hii inamaanisha kuwa mkoa hautasifiwa kwa utulivu pekee, bali kwa kiasi gani umefanikiwa kuvutia mitaji na kutengeneza ajira mpya kwa vijana kupitia sekta binafsi.
Ili kuhakikisha hili halibaki kwenye makaratasi, mfumo mpya wa "Ease of Doing Competitive Business" umezinduliwa. Huu ni mzani wa kidijitali utakaoshindanisha mikoa yote 31 ya Tanzania. Mkoa utakaokuwa na urasimu, utitiri wa tozo, na unaochelewesha vibali vya biashara, utajikuta mkiani mwa orodha hiyo—jambo ambalo ni shinikizo la wazi kwa mamlaka za kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Moja ya matokeo ya haraka ya mkutano wa kihistoria (Mkumbi II) ambao Waziri mkuu alihutubia ni maelekezo ya kufumua utitiri wa kodi na taasisi za udhibiti zinazomtesa mfanyabiashara. Badala ya kusubiri mchakato mrefu wa miaka, Serikali imeamua kuwa kero zote zilizobainishwa na wadau ziingizwe moja kwa moja kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha (Finance Bill) wa mwaka huu.
Hii ni hatua ya kijasiri inayolenga kuondoa 'miiba' barabarani kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya 2050 mwezi Julai. Lengo ni kuhakikisha kuwa sheria hazijengi vikwazo, bali zinakuwa daraja la kukuza uchumi.
Nyuma ya maelekezo haya mazito kuna namba kubwa ambayo ni Dola trilioni moja. Serikali imeweka bayana kuwa ili kukuza uchumi wa Tanzania mara 10 zaidi (kutoka bilioni 100 za sasa), hakuna nafasi ya urasimu wa halmashauri wala tozo zisizo rafiki.
Kimsingi Awamu ya sita imeamua mwelekeo ni mmoja tu: kujenga uchumi wa kisasa, wa kidijitali, na unaojiendesha kibiashara. Hakika ujumbe wa Dodoma ni mweupe—ikiwa wewe ni kiongozi wa umma na huwezi kukuza biashara kwenye eneo lako, unachelewesha safari ya Tanzania kuelekea mwaka 2050.
Social Plugin