
Na Mwandishi Wetu, Tabora
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Anastazia Bebete, amewahimiza wanawake wilayani humo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuongoza familia zao kwa ufanisi, wakimuiga Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amesema anaendelea kuiongoza vyema nchi ya Tanzania.
Bebete alitoa wito huo wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kiwilaya katika Kata ya Ushokola, akisisitiza kuwa wanawake wamepewa uwezo mkubwa wa uongozi na ni muhimu kuutumia ipasavyo kwa maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.
Alisema Rais Samia ni mfano bora wa kuigwa kwa wanawake nchini kwa namna anavyoonyesha uongozi thabiti na kuthibitisha kuwa wanawake wanaweza kuongoza kwa mafanikio wanapopewa nafasi au hata wanapojitokeza wenyewe.
“Hata katika familia, wanawake wamekuwa wakionyesha uongozi mzuri katika malezi na usimamizi wa familia. Wanapokosekana, mara nyingi familia hukosa malezi bora,” alisema Bebete.
Aidha, aliwapongeza wakazi wa Wilaya ya Kaliua kwa kuendelea kumuamini Rais Samia Suluhu Hassan na kumpa ushirikiano unaomwezesha kutekeleza majukumu yake ya kuliongoza taifa.
Bebete, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ushokola, alisema uongozi wa Rais Samia umethibitisha kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kuwa viongozi bora iwapo wataaminiwa na kupewa fursa.
“Hata mimi binafsi nimevutiwa na namna anavyoongoza. Ninaahidi kuendelea kuiongoza vizuri Halmashauri ya Kaliua ili iwe mfano si tu katika Mkoa wa Tabora bali hata kitaifa,” alisema.
Alibainisha kuwa utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo, hususan katika sekta za elimu na afya bila wananchi kulazimika kutoa michango, umechangia kuwapa wanawake nafasi zaidi ya kujihusisha na shughuli za kiuchumi pamoja na kupata muda wa kutosha wa kulea familia zao.
Alisisitiza kuwa wanawake ni nguzo muhimu katika familia, kama ambavyo Rais Samia alivyo nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande mwingine, Bebete alieleza dhamira yake ya kuona Halmashauri ya Kaliua inaendelea kuwa mfano katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma bora kwa wananchi ili halmashauri nyingine ziweze kujifunza kutoka kwao.
Aliongeza kuwa anapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Shaban Kubelwa, wakuu wa idara mbalimbali, watumishi wa halmashauri, madiwani pamoja na wananchi, jambo linalompa nguvu ya kuendelea kuiongoza vizuri halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dk. Gerald Mongela, amewahimiza wanawake wilayani humo kujiamini katika nafasi za uongozi kwa kumuiga Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya urais nchini Tanzania.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Afisa Tarafa wa Kazaroho, Nzuki Sengerema, Dk. Mongela alisema Rais Samia ameonyesha kwa vitendo kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa uongozi, akitaja mafanikio makubwa katika ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya nchini.
Alisema ujenzi wa madarasa, shule, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali umefanyika bila wananchi kutozwa michango, hatua ambayo imewawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za maendeleo bila kuwa na hofu ya michango.
Dk. Mongela pia alieleza kuwa Wilaya ya Kaliua ina bahati ya kuwa na kiongozi mwanamke mchapakazi, akimtaja Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Anastazia Bebete, kuwa ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo wilayani humo na pia mwanamke pekee anayeongoza halmashauri katika Mkoa wa Tabora.
Aliongeza kuwa chini ya uongozi wa Bebete, Halmashauri ya Kaliua imefanikiwa kushika nafasi ya 11 kitaifa katika ukusanyaji wa mapato, na kuwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuendeleza mafanikio hayo.





Social Plugin