Zama za kuona ufugaji ni kazi ya wazee wa vijijini wanaotembea umbali mrefu na fimbo mabegani zimepitwa na wakati, kwani Kampuni ya Mbogo Ranches imekuja na mapinduzi yanayothibitisha kuwa sekta ya mifugo ndiyo "shamba la bibi" jipya kwa vijana wanaotafuta ajira za uhakika.Mkurugenzi Mtendaji wa Mbogo Ranches, Naweed Mulla, ameweka wazi kuwa siri ya kutoboa kiuchumi kuelekea Dira ya 2050 haipo kwenye kuswaga ng'ombe dhoofika, bali ni kuwa mchungaji msomi anayetumia akili, teknolojia, na mbinu za kisasa kunenepesha mifugo na kuvuna faida ndani ya muda mfupi.
Kupitia maonesho makubwa ya mifugo yatakayovuma mwezi Juni mwaka huu, vijana watapata fursa ya kipekee ya kuona namna ufugaji unavyoweza kuendeshwa kama kampuni (startup) yenye mnyororo mpana wa thamani.
Mulla amesisitiza kuwa kijana hahitaji kumiliki ekari mamia kuanza safari hii, kwani Mbogo Ranches inafundisha mbinu za "Feedlot" ambapo unaweza kununua ng'ombe kwenye minada, ukawaweka sehemu moja, ukawapa malisho bora yaliyoongezewa virutubisho, na kuwauza wakiwa na uzito mkubwa ndani ya miezi mitatu pekee, jambo linalofanya mzunguko wa pesa kuwa wa haraka na wenye uhakika.
Sekta hii inatajwa kuwa na fursa lukuki kuanzia kwenye uzalishaji wa nyasi na malisho ya kisasa (hay and silage), utengenezaji wa vyakula vya mifugo, hadi kwenye biashara ya nyama bora inayohitajika kwa wingi kwenye mahoteli na masoko ya nje ya nchi.
Kwa kushiriki maonesho haya ya nne mfululizo, vijana watajionea teknolojia za kidijitali za kusimamia afya ya mifugo na namna ya kupata mitaji, jambo linalofanya ufugaji uonekane kuwa kazi ya hadhi (professional) inayomfanya kijana awe bosi wa maisha yake mwenyewe badala ya kusubiri ajira za maofisini ambazo ni adimu.
Mbogo Ranches imedhamiria kuufanya mwezi Juni kuwa mwanzo wa safari ya mabadiliko kwa vijana wengi, ikiwaaminisha kuwa rasilimali za malisho zilizopo nchini ni dhahabu ya kijani inayoweza kuwatajirisha endapo wataacha mazoea na kukumbatia ubunifu.
Huu ndio msingi wa utekelezaji wa sera ya 2050, ambapo kijana wa Kitanzania anahimizwa kuwa mjasiriamali wa mifugo anayejua thamani ya kila kilo ya nyama na kila lita ya maziwa, akigeuza changamoto za ajira kuwa fursa ya kudumu yenye kipato kisichoyumba.
Social Plugin