Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAPINDUZI YA YOUTUBE TANZANIA: KUTOKA BURUDANI HADI KUWA SOKO KUU LA AJIRA KWA WASANII NA WATENGENEZA FILAMU




Na Beda Msimbe, BSKY Media

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tasnia ya sanaa nchini Tanzania imeshuhudia mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa redio na televisheni.

Jukwaa la YouTube limegeuka kuwa "mhimili mkuu" wa uchumi wa ubunifu, likiondoa utegemezi wa CD, DVD, na hata vituo vya matangazo vya maeneo. Leo hii, mafanikio ya msanii wa muziki au mtengeneza filamu nchini hayapimwi tena kwa kelele za mtaani pekee, bali kwa takwimu za "views," "subscribers," na "watch time."

Wanamuziki: Wafalme wa Algorithm

Wanamuziki wa Tanzania, hususan wa miondoko ya Bongo Flava, wamefanikiwa kupasua anga la kimataifa kupitia YouTube. Kwa sasa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza barani Afrika kwa kuwa na wasanii wenye wafuasi wengi.

Diamond Platnumz, akiwa na zaidi ya wafuasi milioni 8, amekuwa mfano wa namna jukwaa hili linavyoweza kugeuza jina kuwa kampuni. Kutokana na mfumo wa malipo ya matangazo (AdSense), msanii mwenye video inayofikisha views milioni 10 anaweza kuingiza kati ya shilingi milioni 25 hadi 50, kulingana na nchi ambako watazamaji wake wanatoka.

Watengeneza Sinema: Mapinduzi ya 'Web Series' na Shuhuda za Wadau

Kwa upande wa watengeneza sinema, YouTube imekuwa mkombozi baada ya kufa kwa soko la DVD. Hivi sasa, kumezuka wimbi la "Web Series" au tamthilia za mtandaoni ambazo zimejizolea umaarufu mkubwa. Mifano hai ni kama chaneli ya Lamata Village Entertainment na Rk Movies.

Hata hivyo, uhalisia wa soko hili unathibitishwa na sauti za wadau wenyewe ambao wameamua kuwekeza nguvu zao huko. Rafiki yangu wa karibu na msanii wa filamu, Jamillah Mfaume Bode, hivi karibuni alibainisha kuwa kwa sasa anashughulika na mradi mpya (project) mahususi kwa ajili ya YouTube. Jamillah anasisitiza kuwa YouTube imekuwa ndiyo soko kubwa na la uhakika kwa sasa kwa watengeneza maudhui.

Hali kadhalika, muigizaji mahiri Abdul Kingo naye ameamua kufuata mkondo huo kwa kuanzisha chaneli yake binafsi. Kingo anaeleza kuwa amehamishia nguvu zake zote katika kutengeneza kazi bora na kuzirusha kwenye jukwaa hilo, akiamini kuwa huko ndiko kunakomkutanisha na hadhira yake moja kwa moja huku kumlipa kulingana na ubunifu wake. Ushuhuda huu kutoka kwa Jamillah na Kingo ni kielelezo tosha kuwa YouTube si tena jukwaa la majaribio, bali ni soko rasmi lenye ushindani na tija.

Changamoto na Uhusika wa Kiuchumi

Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto. Gharama kubwa ya bando nchini Tanzania inazuia ukuaji wa kasi zaidi. Aidha, watengeneza filamu wanahitaji kuelewa zaidi mifumo ya hakimiliki (Copyright) ili kuzuia kazi zao "kuibiwa" na chaneli nyingine. Hata hivyo, ukweli unabaki kuwa YouTube imetengeneza ajira kwa maelfu ya vijana—kuanzia wapiga picha, wahariri (editors), hadi wasanii wenyewe—na kuifanya sanaa kuwa biashara rasmi inayochangia pato la taifa kupitia uchumi wa kidijitali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com