
Na Lulu Mbwaga - Mwanza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amekabidhi Shilingi Bilioni 7 kwa ajili ya kuwawezesha vijana 308 ambao ni baadhi ya wahitimu wa programu ya BBT (Building a Better Tomorrow) katika sekta ya uvuvi, ili kutekeleza miradi mbalimbali ya ukuzaji viumbe maji.
Vijana hao wanatarajiwa kutekeleza miradi ya ufugaji wa samaki kwa vizimba, ufugaji wa jongoo bahari, unenepeshaji wa kaa pamoja na kilimo cha mwani, ambapo fedha hizo zinatolewa kama mikopo yenye masharti nafuu, sambamba na upatikanaji wa vifaa, pembejeo muhimu za ukuzaji viumbe maji na posho ya kujikimu.
Nanauka amekabidhi fedha hizo Machi 7, 2026 katika viwanja vya Chuo cha Uvuvi Nyegezi mkoani Mwanza, wakati akizindua programu ya kuwezesha mitaji kwa vijana watakaotekeleza miradi ya ufugaji wa samaki kwa vizimba. Miradi hiyo itatekelezwa katika mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera.
Amesema miradi hiyo inayotekelezwa kwa dhana ya uchumi wa buluu inaonesha wazi kuwa vijana wa Kitanzania wana mchango mkubwa katika kusukuma mbele agenda ya Mheshimiwa Rais ya kufanya mageuzi ya kisekta ili kukuza uchumi wa nchi sambamba na kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Nanauka ameeleza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilipoanza safari ya kuwezesha vijana kupitia programu ya BBT mwaka 2022/2023, ilifanya hivyo kwa kushirikiana na iliyokuwa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, jambo lililosaidia kupata vijana mahiri ambao sasa wameanza kunufaika na mitaji hiyo.
Aidha, ametoa wito kwa sekta zote zitakazotekeleza programu za kuwawezesha vijana kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana ili kuhakikisha programu hizo zinafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Napenda kuwahakikishia kuwa hatua hii ya kuwezesha vijana ni endelevu. Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana imetoa mwongozo wa jumla wa namna ya kunufaika na bilioni 200 zilizotolewa na Mheshimiwa Rais. Napongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutoa mwongozo mahususi kuhusu maombi ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 23 kwa ajili ya miradi ya mifugo, uvuvi na ukuzaji viumbe maji kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa,” amesema Nanauka.
Ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais anatarajia kuona kila kijana mwenye sifa anachangamkia fursa hiyo muhimu ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa taifa.
Ikumbukwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2025 aliahidi kutoa Shilingi Bilioni 200 kwa makundi mbalimbali ili kusaidia kuanzisha na kukuza biashara ndogo, za kati na kampuni changa, ambapo tayari fedha hizo zimeanza kuwafikia walengwa.


Social Plugin