Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA KUZINDUA UJENZI WA MATENKI YA KUHIFADHIA MAFUTA DAR ES SALAAM


Na Sheila Ahmadi – Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua ujenzi wa matenki ya kuhifadhia mafuta katika Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha miundombinu ya nishati na uchukuzi nchini.

Akizungumza jijini humo na waandishi wa habari, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema mradi huo utasaidia kupunguza muda wa meli za mafuta kukaa bandarini kutoka wastani wa siku 10 hadi siku 3. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi kwa wawekezaji pamoja na kuimarisha usalama wa nishati nchini.

Profesa Mbarawa ameongeza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa magati katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kubwa za mizigo. Maboresho hayo yataenda sambamba na uimarishaji wa usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), reli ya MGR pamoja na reli ya TAZARA.

Amesema sekta ya uchukuzi inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa taifa kwa kuchangia zaidi ya asilimia 40 ya mapato ya Serikali kupitia kodi ya forodha, pamoja na kuingiza wastani wa dola za Marekani bilioni 2.4 kwa mwaka kama fedha za kigeni kutokana na huduma za uchukuzi kwa nchi jirani.

Aidha, uzinduzi huo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuendeleza na kuboresha bandari ya Dar es Salaam ili iwe lango kuu la biashara na uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Vilevile, mradi huo unatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kimataifa, huku ukiwapa fursa Watanzania kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo.

Kwa upande mwingine, Profesa Mbarawa ametoa wito kwa wafanyakazi wa Tanzania Ports Authority (TPA) kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanaboresha huduma zinazotolewa kwa watumiaji wa bandari hiyo.












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com