Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROF. KABUDI AKUTANA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA BOTSWANA JIJINI LONDON


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Palamagamba J. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Botswana, Mhe. Dkt.Phenyo Butale, jijini London, Uingereza, ambapo viongozi hao wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zao.

Mazungumzo hayo yalifanyika pembezoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Machi 8, 2026 jijini London, ukiwaleta pamoja mawaziri kujadili masuala ya kimataifa na maendeleo ya pamoja.

Viongozi hao wamekubaliana kuendeleza uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Botswana pamoja na kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kielimu kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

Aidha, viongozi hao wamekubaliana kushughulikia kwa pamoja changamoto mbalimbali zinazoibuka katika mazingira ya kimataifa yanayobadilika kwa kasi, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya teknolojia, mabadiliko ya kiuchumi pamoja na mwenendo wa kisiasa duniani.

Prof. Kabudi aliambatana na Mshauri wa Rais katika masuala ya diplomasia, Balozi Lazaro Nyarandu; Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Mbelwa Kairuki; pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Noel Kaganda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com