Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAAFISA UDAHILI NA MITIHANI WA VYUO TANZANIA WAPEWA MBINU KUIMARISHA HUDUMA


Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog

Mafunzo maalum ya Maafisa Udahili na Maafisa Mitihani kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini, yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), yamehitimishwa leo Februari 5, 2026 katika Ukumbi wa NSSF, Manispaa ya Shinyanga.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliwakutanisha maafisa kutoka vyuo mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa mifumo ya udahili na mitihani, kuongeza uelewa wa taratibu na kuboresha utoaji wa huduma kwa wanafunzi.

Katika siku hizo mbili za mafunzo, washiriki waliwasilishiwa mada mbalimbali zilizojikita katika matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki ya NACTVET, taratibu za udahili wa wanafunzi, usimamizi wa mitihani pamoja na upakiaji wa matokeo kwa kuzingatia miongozo na kalenda ya kitaaluma ya Baraza.

Mada hizo zililenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Maafisa Udahili na Mitihani, kupunguza changamoto za ucheleweshaji wa taarifa katika kanzidata ya NACTVET na kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma kwa wakati ikiwemo mikopo ya elimu, vyeti na fursa za ajira.

Aidha, washiriki wamepata fursa ya kujadili kwa vitendo changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utendaji kazi kwa kuzingatia miongozo na kanuni za Baraza.

Kupitia mafunzo hayo, NACTVET imedhihirisha dhamira yake ya kuendelea kuimarisha uwezo wa rasilimali watu katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, hatua inayolenga kuboresha ubora wa elimu, utoaji wa huduma na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com