Na Regina Ndumbaro -Namtumbo
Watumishi wawili wa umma katika Kata ya Lusewa, Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma wamejikuta wakikalia kuti kavu na kutakiwa kupangiwa vituo vingine vya kazi baada ya wananchi kutoa malalamiko dhidi ya watumishi hao kukiuka maadili ya kazi.
Hatua hiyo imekuja wakati wa ziara ya Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Dkt. Juma Zuberi Homera kufika katika kata ya Lusewa na kumuachia jukumu hilo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kusimamia kwa karibu hatua za kinidhamu dhidi ya mhudumu mmoja wa kituo cha afya cha Lusewa, Peter Ndunguru, kwa tuhuma za kuwatoza wagonjwa fedha kinyume cha sheria, pamoja na Mtendaji wa Kata ya Lusewa, Wyclife Mulinda, kwa kushindwa kushirikiana vyema na wananchi.
Dkt. Homera amesisitiza kuwa ni marufuku kwa watumishi wa afya kuwatoza wananchi fedha wanapopata huduma, akiwataka wananchi kutoa taarifa mapema pindi wanapoona ukiukwaji wa maadili au uzembe wa viongozi wao.
Katika ziara hiyo,Dkt Homera amekabidhi gari la wagonjwa (ambulance) kwa kituo cha afya cha Lusewa, akionya lisitumike kwa matumizi mengine yasiyo ya afya na kusisitiza kuwa wagonjwa hawapaswi kutozwa nauli.
Aidha, ametoa taarifa ya wahudumu wapya kufika katika kijiji hicho ambao ni madaktari wawili na wahudumu wanne wa afya, pamoja na kuomba Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la OPD na kituo cha afya kutokana na majengo ya sasa kuwa chakavu.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO), Dkt. Aaron Hyera, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dkt. Homera kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuboresha sekta ya afya.
Amesema kupatikana kwa ambulance kutasaidia sana kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto, hasa wanaotoka maeneo ya mbali.
Dkt. Hyera amekiri kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya watoa huduma kukiuka sera ya huduma bure kwa wajawazito na watoto wachanga (M-MAMA), na kuahidi kuchukua hatua pamoja na kuhakikisha gari hilo linalindwa na kutumika kwa wagonjwa pekee.
Wananchi wa kijiji cha Lusewa wameeleza furaha yao, wakiongozwa na Sharifu Ibadi Alufajiri aliyesema ujio wa Dkt. Homera na kupatikana kwa ambulance kumeondoa adha kubwa ya wagonjwa kulazimika kutumia magari ya abiria.
Hata hivyo, wameeleza changamoto ya majengo ya kituo cha afya kuwa chakavu na wodi kuwa ndogo, hususan wodi ya wanaume na ya mama na mtoto.
Mkazi mwingine, Dalia Ali Katambo, amepongeza utekelezaji wa ahadi ya gari la wagonjwa (ambulance) na kuomba Serikali iendelee kuwasaidia, ikiwemo kushughulikia changamoto za ajira kwa vijana, akisisitiza kuwa bado wana imani kubwa na Mbunge wao katika kutatua kero za wananchi wa Lusewa.




Social Plugin