Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHILATU AWAPONGEZA WANANCHI KUUNGANA NA SERIKALI

~ Awapongeza Wanafunzi kuripoti shuleni 

~ Aridhishwa na upatikanaji wa Chakula Shuleni

Na Mwandishi Wetu

Afisa Tarafa wa Lisekese mkoani Mtwara, Emmanuel Shilatu, amewapongeza wazazi, wanafunzi na wananchi kwa ujumla kwa kuungana na Serikali katika kuhakikisha wanafunzi wanaripoti shuleni kwa wakati.

Shilatu aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kujiridhisha na hali ya uripoti wa wanafunzi shuleni, ambapo alieleza kuridhishwa na mwitikio mkubwa wa wanafunzi pamoja na hali ya upatikanaji wa chakula shuleni. 

Katika ziara hiyo, alitembelea shule za msingi, sekondari pamoja na shule maalum na kujionea uwepo wa chakula na mboga, huku wanafunzi wakipata uji na chakula cha mchana katika shule zote alizotembelea.

“Nawapongeza sana wanafunzi wote walioripoti shuleni mapema, lakini zaidi nawapongeza wazazi kwa kuitikia wito wa Serikali na kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni,” alisema Shilatu.

Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza kwa vitendo sera ya elimu bure pamoja na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya shule.

“Kwa sasa kuna madarasa ya kutosha, madawati, vifaa vya kisasa vya maabara pamoja na uwepo wa walimu. Niwaombe wananchi waendelee kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisisitiza.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi waliokuwa shuleni wakiwapeleka watoto wao, Iyvone Dihenga aliipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu ya shule na kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha watoto kuripoti shuleni kwa urahisi.

Alisema hali hiyo imechochea wazazi wengi kujitokeza kwa wingi kuungana na Serikali katika kuhakikisha watoto wao wanapata elimu.

Kwa upande mwingine, wanafunzi kote nchini walifungua shule rasmi tarehe 13 Januari 2026, huku Serikali ikiendelea kusisitiza kuwa elimu ni bure na kwamba mwanafunzi yeyote apokelewe shuleni bila kikwazo chochote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com