Na Michael Abel - Shinyanga
Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea asubuhi ya leo Januari 27, 2026, katika eneo la Mnadani, Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Ajali hiyo imehusisha basi la abiria la kampuni ya KISIRE lenye namba za usajili T 229 EEL, lililokuwa likitoka Kahama kuelekea Mwanza, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa limebeba shehena ya mchele kutoka Dar es Salaam kwenda Rwanda lenye namba za usajili RAE 849N.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amesema aliyefariki ni dereva wa lori hilo, huku majeruhi 12 wakikimbizwa Hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Amesema kati ya majeruhi hao, 5 wapo katika hali mbaya na wanaendelea kupatiwa huduma za dharura chini ya uangalizi wa madaktari bingwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga huku wengine 7 wakipatiwa matibabu katika kituo cha afya Tinde.
Kamanda Magomi amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe na mwendokasi, unaodaiwa kufanywa na dereva wa basi alipokuwa akijaribu kulivuka lori lililokuwa mbele yake katika jaribio la kukwepa mkokoteni uliokuwa umebeba matikiti kuelekea mnadani na kusababisha ajali hiyo.







Social Plugin