
Timu ya Taifa ya Senegal, maarufu kama Lions of Teranga 'Simba wa Teranga', imeandika historia mpya baada ya kutwaa ubingwa wa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika fainali kali iliyochezwa usiku wa Januari 18, 2026 nchini Morocco.
Mchezo huo uliwakutanisha wababe wawili wa soka barani Afrika, huku kila timu ikionesha kiwango cha juu, nidhamu ya kiufundi na mapambano ya hali ya juu.
Dakika 90 za kawaida ziliisha bila mshindi kutokana na uimara wa safu za ulinzi na makipa wa pande zote mbili, hali iliyosababisha kuchezwa kwa dakika 30 za muda wa nyongeza.
Dakika ya 107, mashabiki wa Senegal walilipuka kwa furaha baada ya mshambuliaji Pape Alassane Gueye kufunga bao la ushindi, bao lililodumu hadi filimbi ya mwisho na kuipa Senegal taji lao la pili la AFCON katika historia ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Kwa mafanikio hayo, Senegal imejinyakulia zawadi ya Dola za Kimarekani Milioni 10 (sawa na takriban Shilingi Bilioni 24.7 za Kitanzania), ikiwa ni ongezeko kubwa la fedha za zawadi ikilinganishwa na AFCON 2023, hatua inayolenga kuinua ushindani na hadhi ya mashindano hayo.
Kwa upande wao, wenyeji Morocco walioshindwa katika fainali hiyo wamepokea Dola Milioni 4, kama ilivyotangazwa na Rais wa CAF Patrice Motsepe, ikiwa ni sehemu ya mpango wa CAF kuongeza motisha kwa timu zinazofika hatua za juu.
Matokeo hayo yanaifanya Morocco kupoteza fainali ya pili ya AFCON katika historia yao, baada ya mara ya kwanza kufanya hivyo mwaka 2004 walipopoteza dhidi ya Tunisia.
Senegal sasa inajiweka kwenye ramani ya mataifa makubwa ya soka Afrika, ikithibitisha uimara na ubora wake katika anga la soka la bara hilo.
Social Plugin