Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa utafiti wa mafuta na gesi asilia katika kitalu cha Eyasi–Wembere, kinachojumuisha mikoa mitano ya Simiyu, Singida, Arusha, Shinyanga na Tabora, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu nchini.
Mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Meatu (Simiyu), Iramba na Mkalama (Singida), Karatu na Ngorongoro (Arusha), Kishapu (Shinyanga) pamoja na Igunga (Tabora), ukiwa na lengo la kuongeza vyanzo vya nishati (energy mix) kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kambi ya Utafiti iliyoko katika kijiji cha Endesh, wilayani Karatu, Meneja Mradi, Mjiofizikia Sindi Maduhu, amesema utekelezaji wa mradi huo unatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, inayoipa TPDC jukumu la kufanya utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia nchini.
Maduhu amesema kuwa katika awamu ya pili ya mradi, TPDC inaendelea na ukusanyaji wa taarifa za mitetemo (2D seismic data acquisition) kwa kutumia vilipuzi, hatua inayotokana na hali ya kijiografia ya maeneo yaliyosalia, yaliyoko katika ukanda wa ziwa Eyasi na kitangiri na maeneo oevu yanayohitaji mbinu maalum za kitaalamu.
“Awamu ya pili ya mradi ilianza rasmi mwezi July 2024 ambapo asilimia 47 tulitumia magari maalum ya mitetemo na kufikia juni 2025 tulianza maeneo yenye ziwa kwa kutumia vilipuzi. Hadi sasa imefikia takribani asilimia 69 ya utekelezaji, huku gharama za jumla zikifikia Shilingi bilioni 28,” amesema Maduhu.
Ameongeza kuwa mradi huo umeleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii zinazozunguka maeneo ya utekelezaji, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa takribani vijana 1000 kutoka maeneo husika, sambamba na utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Miradi hiyo ya kijamii imejumuisha uchimbaji wa visima vya maji, ujenzi wa malambo ya mifugo pamoja na ugawaji wa vifaa vya michezo katika shule za msingi na sekondari, hatua inayolenga kuboresha huduma za kijamii na ustawi wa wananchi.
Hata hivyo, Maduhu amesema mradi huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, ambapo maeneo yaliyotarajiwa kuwa na maji yamekauka na kusababisha vifaa vilivyoandaliwa kwa ajili ya kutumika kwenye maeneo hayo kushindwa kufanya kazi , hali inayoongeza ugumu na gharama katika zoezi la ukusanyaji wa taarifa za utafiti.
Licha ya changamoto hizo, TPDC imeeleza kuwa itaendelea kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, usalama na ulinzi wa mazingira, ili kuhakikisha malengo ya kitaifa ya utafiti na maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi yanafikiwa kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.





















Social Plugin