Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA NA CHINA ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA KISHERIA KIUCHUMI NA TEKNOLOJIA


Na Mwandishi Wetu Malunde 1-Blog 

Dkt. Juma Zuberi Homera Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, amekutana na  Chen Mingjian, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, katika jengo la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) jijini Dar es Salaam. 

Mkutano huo umelenga kuimarisha na kuendeleza mashirikiano ya kirafiki na kimaendeleo kati ya Tanzania na China katika nyanja mbalimbali za kipaumbele.

Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Katiba na Sheria amewasilisha ombi la kuendelezwa kwa mashirikiano na kubadilishana uzoefu katika masuala ya kisheria, ikiwemo uboreshaji wa mifumo ya utoaji haki, haki za binadamu na matumizi ya teknolojia za kisasa. 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kujifunza mbinu za kukuza uchumi, hususan kupitia matumizi ya uchumi wa kimtandao (e-commerce) kama chachu ya maendeleo.

Kwa upande wake, Balozi wa China ameeleza kuwa Serikali ya China iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya kisheria, e-commerce na sekta nyingine za kimkakati kwa manufaa ya pande zote. 

Mkutano huo unaakisi dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kisheria, kukuza matumizi ya teknolojia na kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wote kupitia mashirikiano ya kimataifa.Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Zuberi Homera 




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com