Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Katika maeneo kame ya Mkoa wa Dodoma, ambako mvua imekuwa haitabiriki kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, jua ambalo kwa miaka mingi lilionekana kama adui wa kilimo sasa limegeuka kuwa suluhu ya matumaini mapya.
Wakulima wa kilimo cha umwagiliaji, waliokuwa wakiteseka kutokana na gharama kubwa za mafuta ya petroli na dizeli, sasa wanapitia mageuzi makubwa baada ya wakulima kuanza kutumia nishati ya jua kuendesha pampu za maji hatua inayopunguza gharama za uzalishaji na kuongeza uwezekano wa mavuno ya uhakika.
Mpunguzi, Kata ya Matumbulu, ni moja ya maeneo yanayoongoza katika mabadiliko haya, ambapo wakulima ambao zamani walitegemea mafuta sasa wanageukia teknolojia ya umeme jua kama njia mbadala ya maisha.
Matayo Kusenha anasema kwa miaka mingi, kilimo katika maeneo hayo kilikuwa kimefungwa kwenye mzunguko wa gharama kubwa za mafuta.
Anasema alilazimika kutumia sehemu kubwa ya mapato yake kununua petroli ili kuendesha pampu za maji, hali iliyopunguza faida na wakati mwingine kuwakatisha tamaa ya kuwekeza zaidi katika kilimo.
Naye Mathias Chisesa, mkulima wa nyanya katika shamba la nusu ekari, anasema hali hiyo ilikuwa changamoto ya kila msimu.
“Kilimo chetu kinategemea umwagiliaji kwa sababu mvua hazitoshelezi,tunatumia pampu za petroli, lakini gharama za mafuta zinabadilika kila mara wakati mwingine faida inamezwa na mafuta,” anasema.
Kwa mujibu wake, wakati mwingine hulazimika kuwasha pampu kila baada ya siku mbili au tatu, hali inayosababisha kilimo kuwa cha kubahatisha badala ya kuwa biashara yenye uhakika.
Afisa Kilimo wa Kata ya Matumbulu, Aneth Mnana, anathibitisha kuwa umwagiliaji sasa ndiyo nguzo kuu ya uzalishaji katika maeneo hayo kutokana na mvua kutokuwa na uhakika.
“Wakulima wengi hapa wanategemea umwagiliaji,bila umwagiliaji, uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara unakuwa mgumu sana,” anasema.
Kauli hiyo inaweka wazi ukweli kwamba kilimo cha Dodoma sasa hakitegemei tena bahati ya mvua, bali teknolojia na uwekezaji wa nishati mbadala.
Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Wizara ya Kilimo imeongeza juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu, hususan umeme jua, kama njia ya kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija.
Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila, anasema nishati ya jua ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuhakikisha upatikanaji wa nishati endelevu.
“Sekta ya nishati inaendelea kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa shughuli za kijamii na uzalishaji, na umeme jua ni sehemu muhimu ya mabadiliko haya,” anasema.
Kwa upande wa sekta ya umwagiliaji, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) inaeleza kuwa miradi ya visima na mifumo ya kisasa inaendelea kuongezwa ili kuruhusu wakulima kutumia pampu za sola.
Mhandisi Naomi Mcharo anasema miradi hiyo inalenga kuongeza eneo linalomwagiliwa na kuboresha tija ya kilimo nchini.
“Tunaendelea kutekeleza miradi ya umwagiliaji kwa kuchimba visima na kuweka miundombinu inayowezesha wakulima kutumia teknolojia mbalimbali kulingana na mahitaji yao,” anasema.
Tanzania inalenga kufikia zaidi ya hekta milioni 1.2 za umwagiliaji kama sehemu ya mkakati wa usalama wa chakula na kilimo cha biashara.
Licha ya matumaini mapya, changamoto kubwa bado ni gharama za awali za kufunga mifumo ya umeme jua.
Wakulima wengi wanaunga mkono teknolojia hiyo lakini wanashindwa kuimudu kifedha.
Mussa Malogo, mkulima wa mboga mboga, anasema mabadiliko hayo ni muhimu lakini bado hayajafika kwa wote.
“Tunataka sana kuhamia kwenye sola, lakini gharama za awali ni kubwa sana kwa mkulima wa kawaida,” anasema.
Naye Anna Raphaeli anaeleza kuwa gharama za mafuta zimekuwa zikipunguza faida ya kilimo kwa miaka mingi.
“Fedha nyingi zinakwenda kwenye mafuta. Tukipata sola itakuwa nafuu sana,” anasema.
Sekta binafsi imeanza kuchangamkia fursa ya ongezeko la mahitaji ya teknolojia ya umeme jua vijijini na maeneo ya kilimo.
Mkurugenzi wa Dom Energy Solutions, Anthony Machai, anasema kuna mabadiliko makubwa ya fikra kwa wakulima.
“Wakulima sasa wanaona faida ya muda mrefu ya sola kwa sababu gharama za uendeshaji zinapungua sana baada ya uwekezaji wa awali,” anasema.
Hali hii inaonyesha kuwa mabadiliko ya nishati si tu ya kisera, bali pia ya kibiashara na kijamii.
Mtaalamu wa kilimo, Dkt. Kenneth Nzowa, anasema changamoto kubwa iliyobaki ni elimu na upatikanaji wa mitaji nafuu.
Anasisitiza kuwa bila maarifa sahihi na mifumo ya kifedha, wakulima wengi wataendelea kubaki nyuma licha ya uwepo wa teknolojia bora.
Mageuzi ya nishati ya jua katika kilimo cha umwagiliaji Dodoma yanaonyesha picha mpya ya mapambano ya mkulima wa ukame kutoka utegemezi wa mafuta hadi uhuru wa nishati endelevu.
Hata hivyo, safari bado haijakamilika. Changamoto za gharama za awali na upatikanaji wa mitaji zinahitaji suluhu ya pamoja kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi za kifedha.
Lakini kwa wakulima wa Mpunguzi, jua ambalo lilikuwa chanzo cha ukame sasa linageuka kuwa chanzo cha maisha, matumaini na mapinduzi ya kilimo cha kisasa.




Social Plugin