Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADIWANI WAMPIGIA KURA ZA HAPANA MGOMBEA PEKEE UENYEKITI HALMASHAURI MJI WA BARIADI




Zebedayo Lazaro Kingi

Madiwani wateule kupitia chama cha mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wamekataa kupitisha jina la Zebedayo Lazaro Kingi aliyeteuliwa na chama hicho kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.

Katika uchaguzi huo wa kura za maoni ambao umefanyika leo, Mgombea huyo amepata kura 4 za ndiyo na kura za Hapana 11 kati ya kura 15 zilizopigwa.

Baadhi ya madiwani ambao wameshiriki uchaguzi huo (majina yanahifadhiwa) wamedhibitishwa matokeo hayo huku wakieleza kuwa Diwani huyo hakuwa chaguo lao.

“ Kamati ya siasa ilipendekeza majina mawili na hili la huyu likiwemo, lakini baada ya michakato ndani ya chama tukaletewa jina moja, ambapo tulitakiwa kupiga kura ya ndiyo na hapana, na huyu hakuwa chaguo letu tukaamua kupiga ya hapana, tumemkataa hatumtaki,” amesema mmoja wa Diwani.

Alipotafutwa na waandishi wa Habari Katibu wa CCM Wilayani Ibrahimu Kijanga ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huyo, amesema uchaguzi huo ilikuwa moja ya  michakato ya chama hicho ya ndani.

“ Siwezi kutoa matokeo, hii ilikuwa moja ya mchakato wa ndani ya chama chetu, tumemaliza uchaguzi na sasa tunaelekea katika hatua nyingine ndani ya chama,” amesema Kijanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com