Diwani wa Kata ya Mshangano Benson Sovella akiwa pamoja na wanakikundi wa Mlimani Park mtaa wa Namanyigu kata ya Mshangano Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Kikundi cha wajasiriamali cha Mlimani Park, kilichopo mtaa wa Namanyigu kata ya Mshangano, kimeweka rekodi ya kuwa miongoni mwa vikundi vilivyopata mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu.
Kikundi hicho chenye jumla ya wanachama 32 kimejikita katika maendeleo na mshikamano, kikiwasaidia wanachama wake katika nyakati za changamoto na sherehe.
Kupitia juhudi zao, wamefanikiwa kununua eneo la nusu ekari kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi wa mikutano na biashara ya ukodishaji, pamoja na kununua pikipiki mbili za matairi matatu (GUTA), maturubai, na kuwa na akiba ya shilingi milioni saba.
Kutokana na mafanikio hayo, kikundi hicho kilimkaribisha Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mshangano, Benson Sovella, kutembelea na kujionea miradi yao ikiwemo kiwanja cha ujenzi wa ukumbi wa mikutano na vifaa walivyonunua.
Diwani Sovella amewapongeza wanakikundi hao kwa bidii na maendeleo yao, akiwashukuru kwa kumuamini na kumpa kura za kumchagua, huku akisisitiza kuwa yeye ni kiongozi wa wananchi wote.
Aidha, Sovella amegusia masuala muhimu ya afya, mikopo, miundombinu ya barabara, pamoja na huduma za umeme na maji katika mtaa wa Namanyigu.
Kwa upande wao, wanakikundi wa Mlimani Park akiwemo Hamisi Mapunda na Halima Gerodi Mapunda, wameeleza kufurahishwa na mwitikio wa Diwani Sovella kuitikia mwaliko wao.
Wamesema kuwa kila mwishoni mwa mwaka hukutana kutathmini mafanikio yao na pia walitumia fursa hiyo kutoa changamoto walizonazo, hasa katika sekta za afya, umeme, kivuko na maji.
Wamemuomba diwani huyo kuzifanyia kazi changamoto hizo, wakisisitiza kuwa hawakupoteza kura zao na wako tayari kushirikiana naye bega kwa bega katika kuleta maendeleo ya kata yao.

Social Plugin