Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na Diwani wa Kata ya Ndoleleji Mhe. Josephat E. Limbe akizungumza kwenye kikao cha kwanza cha baraza la madiwani kilichofanyika Disemba 3,2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo
Na Sumai Salum-Kishapu
Kikao cha Baraza la Madiwani Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kilichojaa hamasa, umoja na taswira mpya ya kiuongozi, kimefanyika Disemba 3, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu. Kikao hicho kimeacha alama mpya baada ya madiwani kuchagua viongozi wapya watakaoliongoza Baraza kwa kipindi kijacho.
Katika hatua iliyopokelewa kwa shangwe, Diwani wa Kata ya Ndoleleji, Mhe. Josephat Emmanuel Limbe, alichaguliwa rasmi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, huku Diwani wa Kata ya Masanga, Mhe. Enock Reuben Bundala, akivishwa jukumu la Makamu Mwenyekiti. Uchaguzi huo umetafsiriwa kama mwanzo mpya unaohitaji uwajibikaji, maarifa na uadilifu wa hali ya juu.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe.Peter N.Masindi akizungumza kwenye kikao cha kwanza cha baraza la madiwani kilichofanyika Disemba 3,2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, akitoa nasaha, amewapongeza viongozi hao huku akiwakumbusha thamani ya imani waliyopewa na wananchi wa Kishapu.
“Nafasi mliyopewa ni dhamana nzito. Wajibu wenu, kama madiwani, ni kuhakikisha mnasikiliza na kutatua kero za wananchi. Shirikianeni na watendaji wenu, walindeni na kuwaongoza kwa weledi, maana ninyi ndiyo viongozi wanaowaongoza katika maeneo mnayoyasimamia,” ameongeza Mhe. Masindi.
Masindi amesisitiza pia kwamba viongozi hao waende kinyume na mazoea ya kujihusisha na maslahi binafsi, badala yake waweke mbele ustawi wa wananchi na ufanisi wa miradi ya Serikali.
“Jiepusheni kabisa na maslahi binafsi kwenye miradi ya Serikali. Vunjeni makundi ya kisiasa ya kabla ya uchaguzi, mkumbatie wawekezaji, na zingatieni mipaka ya utendaji. Kishapu tunataka iwe mfano wa utawala bora,” ameongeza.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya, Fatma Mohammed, aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa kikao kabla ya kuapishwa na kuchaguliwa kwa Mwenyekiti mpya, amewapongeza madiwani kwa kukamilisha uchaguzi na kuwataka waende kwenye hatua ya utekelezaji.
“Wananchi wamewachagua kwa imani kubwa. Huu sio wakati wa maneno tena ni wakati wa kazi. Tekelezeni yale mliyoyaahidi wakati wa kampeni,” amesema Fatma
Akizungumza kwa hisia za shukrani baada ya kuchaguliwa, Mhe. Josephat Limbe ameahidi kuongoza Baraza hilo kwa uadilifu, weledi na misimamo inayojenga mustakabali wa wananchi wa Kishapu.
“Ninaamini katika kazi za pamoja. Tumepata dhamana ya kuwatumikia wananchi, na tutahakikisha tunasimamia maelekezo ya Mheshimiwa Rais na maazimio ya Baraza letu. Nawaomba watumishi: tufanye kazi kwa bidii, nidhamu na uwajibikaji,” amesema Limbe.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Emmanuel Johnson, amewataka madiwani kuimarisha ushirikiano katika ngazi zote za utendaji ili kujenga mazingira mazuri ya kazi na maendeleo.
“Ili tuijenge Kishapu tunayoiota, lazima tushirikiane. Fanyeni maamuzi kwa kuzingatia mapato halisi ya Halmashauri, sikilizeni wananchi wanachotaka, na tumieni busara katika kushughulikia makosa ya watumishi. Mko hapa kuwaongoza, kuwashauri na kuwaweka kwenye mstari,” amesisitiza Mkurugenzi Johnson.
Pia amewakumbusha umuhimu wa kuzifahamu kwa kina kanuni za Halmashauri, sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma ili kuhakikisha utendaji wenye uadilifu na uwazi.
Katika hatua ya mwisho ya kikao hicho, madiwani waliapishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kishapu, Bi. Johanita Projest, na kisha kuunda kamati za kudumu za Halmashauri ambazo ndizo mhimili wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Social Plugin