Diwani wa Kata ya Ngokolo, Jackline Isaro, ameanza rasmi majukumu yake baada ya kula kiapo cha udiwani leo Desemba 4, 2025, akiahidi kusimama imara katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo ndani ya Baraza la Madiwani la Manispaa ya Shinyanga.
Isaro, akiwa miongoni mwa madiwani wapya walioapishwa, amesema anaingia kwenye baraza hilo akiwa na dhamira ya kufanya kazi kwa kushirikiana na madiwani wote bila kujenga makundi, jambo lililoonekana bayana katika uchaguzi wa viongozi wa halmashauri uliofanyika siku hiyo.
Katika uchaguzi huo, uliosimamiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, Said Kitinga, Baraza la Madiwani limemchagua Salum Kitumbo kuwa Mstahiki Meya na Pendo Sawa kuwa Naibu Meya, wote kwa kura 23 za ndiyo ishara ya umoja ulioimarika ndani ya baraza hilo.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa, Isaro amesema: “Nimeapa kufanya kazi kwa maslahi ya wananchi wa Ngokolo na Manispaa kwa ujumla. Sitakuwa diwani wa maneno, bali wa matendo. Umoja wetu kama madiwani ndiyo silaha ya kuharakisha maendeleo.”
Uapisho huo umeongozwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Chibe, Mh. Agness Mlimbi, aliyewataka madiwani kuzingatia katiba, kanuni na maadili ya uongozi, akisisitiza kuwa wananchi wanahitaji matokeo na sio visingizio.
Baada ya viapo, baraza limeendelea na hatua ya kuunda kamati za kudumu nguzo kuu za kusimamia miradi, mipango, bajeti na uwajibikaji wa halmashauri.
Madiwani wote, akiwemo Jackline Isaro, wanatarajiwa kuanza kazi mara moja katika kamati hizo ili kuhakikisha kasi ya utendaji haiwi ya kusuasua.
Soma pia
Diwani wa Kata ya Ngokolo, Jackline Isaro akiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani
Diwani wa Kata ya Ngokolo, Jackline Isaro akila kiapo kwenye kikao cha baraza la madiwani
Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga, Salum Kitumbo
Naibu Meya Manispaa ya Shinyanga , Pendo Sawa
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mwl. Alexius Kagunze
Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga, Saidi Kitinga































Social Plugin