Kutokana na wito wa baadhi ya wachochezi wa kisiasa kuitisha maandamano mnamo Desemba 9, 2025, sauti za wananchi na viongozi wa dini zimeibuka zikisisitiza umuhimu wa amani, utulivu, na kukataa kabisa vurugu zozote zinazoweza kutishia usalama wa taifa.
Kumbukumbu ya matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025, wakati wa uchaguzi, inatajwa na wengi kama funzo tosha linalothibitisha kuwa vurugu hazina nafasi katika ujenzi wa taifa.
Kauli ya Askofu Mollel: Desemba 9 ni Siku ya Kupumzika
Askofu Mollel ametoa wito kwa Watanzania kutotoka majumbani kwa ajili ya maandamano hayo, akisisitiza kuwa Desemba 9 ni siku iliyopangwa kwa ajili ya kupumzika.
"Watanzania wasitoke siku ya Desemba 9 kwani ni siku ya kupumzika. Wawaambie na watoto wao wasitembee. Hali ya amani na utulivu ni muhimu," alisema Askofu Mollel.
Sauti za Wananchi Zinasisitiza Ujenzi wa Taifa
Wananchi kutoka mikoa mbalimbali wameeleza jinsi hali ya utulivu ilivyo muhimu baada ya Uchaguzi Mkuu, wakisema inajenga mazingira bora kwa maendeleo.
Happiness Mkubilu, Mkazi wa Tunduma, alibainisha umuhimu wa amani baada ya uchaguzi:"Kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na amani na utulivu baada ya uchaguzi, amani baada ya uchaguzi hujenga mazingira bora ya serikali kuwajibika kwa ahadi ilizozitoa wakati wa kampeni kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo wanayostahili.
Pia, hali ya utulivu huchochea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ufanisi, kwa sababu serikali inakuwa na muda na nguvu ya kushughulikia maendeleo badala ya kutumia muda wake kutuliza vurugu."
Jerse Mwang’onda, Mkazi wa Songwe, alieleza namna amani inavyosaidia kuponya tofauti:"Amani ni muhimu zaidi kwa wakati huu baada ya yaliyotokea wakati wa uchaguzi kwani inasaidia kuleta mshikamano wa kitaifa, kuponya tofauti za kisiasa, na kuweka msingi wa ushirikiano kati ya viongozi waliochaguliwa na wananchi. Bila amani, hakuna maendeleo, na bila ushiriki wa amani katika uchaguzi, demokrasia haiwezi kukua ipasavyo."
Thokozan Mwangosi, Mkazi wa Ileje, alitoa onyo kuhusu athari za migogoro:"Sisi Watanzania bado tunahitaji maendeleo ya kweli kwenye nchi yetu, hivyo tunapaswa kudumisha amani kipindi hiki na tujiepushe na migogoro isiyo ya lazima baina ya mtu na mtu, familia na familia hadi kufika kwenye ngazi ya taifa tusije kufikia tukawa wakimbizi kwenye nchi yetu wenyewe."
Ya Oktoba 29 inatosha
Kauli za wananchi hawa zote zinarejelea matukio ya vurugu ya Oktoba 29, 2025, yakisisitiza kuwa machafuko hayo yanatosha na hayapaswi kujirudia. Badala yake, Watanzania wanashauriwa kuzingatia hali ya amani na utulivu iliyopo, huku wakitaka nguvu zote zielekezwe katika kuisaidia serikali kufanya kazi na kutekeleza ahadi zake za maendeleo.

Social Plugin