Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDUMBARO AAHIDI MAPINDUZI YA MAENDELEO SONGEA MJINI



Na Regina -Songea -Ruvuma

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Songea Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Damasi Ndumbaro, ameahidi kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii ikiwa atachaguliwa kuongoza jimbo hilo.

Akizungumza leo Agosti 14, 2025 katika viwanja vya Kiblang’oma, Kata ya Lizaboni wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu, Dkt. Ndumbaro amesema serikali ya CCM itaweka kipaumbele katika kusambaza umeme katika kila kaya Songea Mjini, pamoja na kuhakikisha ujenzi wa nyumba bora katika maeneo yaliyopimwa kisheria.

Dkt. Ndumbaro pia ameeleza kuwa ujenzi wa masoko ya kisasa Manzese A na B ni moja ya ajenda zake kuu, pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara.

Amefafanua kuwa tayari wakandarasi wamelipwa na fidia kwa ajili ya ukarabati wa barabara zenye urefu wa kilomita 100 kuanzia Mtukira, pamoja na barabara ya Mtwara-Kordo (km 14), inayopita Kata ya Mshangano hadi Msamala na kuunganishwa na barabara ya Ruhuwiko.

Aidha, ahadi zilitolewa za kujenga barabara muhimu kama ya London hadi Subira, Msamala hadi Mwengemshindo kwa kiwango cha lami, na barabara ya Mshangano hadi Mletele.

Katika nyanja nyingine za maendeleo, Dkt. Ndumbaro ameahidi kuboresha uwanja wa ndege wa Songea na kuimarisha sekta ya michezo kwa lengo la kuirejeshea heshima Songea kama kitovu cha michezo nchini.

Amesisitiza kuwa Songea ina kasi kubwa ya ukuaji na ni mji wa kwanza unaokua kwa haraka nchini, hivyo ana azma ya kuhakikisha inapata hadhi ya kuwa Jiji kamili.

Amewaomba wananchi kumpa ridhaa ili kuleta maendeleo ya kweli kupitia CCM.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com