
Na Faustine Kasala - Kigoma
Mgombea Ubunge jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama cha Alliance for change and Transparency ACT wazalendo, Zitto Kabwe amesema ataendeleza safari aliyoishia Mwaka 2020 katika kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Kigoma Mjini katika hatua mbalimbali za maendeleo endapo ataaminiwa kwa mara nyingine wananchi wa Jimbo hilo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kampeni za Chama hicho uliofanyika katika uwanja wa Mwami Luyagwa kata ya Gungu Manispaa ya Kigoma Ujiji Zitto amesema amejipanga kuhakikisha miradi yote ya maendeleo iliyo kwama katika Jimbo hilo na maeneo mengine ya mkoa wa Kigoma inakamilika kwa kiwango kinachotakiwa.

“Nawaombeni wana Kigoma mjini nirudisheni tena Bungeni ili turejeshe heshima ya Jimbo letu na Mkoa wetu kwa ujumla! na niwaahidi, nimejipanga kuhakikisha nasimamia masuala ya kilimo na Miundombinu,mfano kukamilisha mpango wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la mto Luiche, Kurejesha miradi ya Barabara za Mitaa Barabara ya Kasulu na Mifereji ya maji ya Mvua” ,amesema Zitto.

Aidha Zitto katika Hotuba yake ameahidi kuifanya Kigoma kuwa kituo kikuu cha Biashara na lango la Maziwa Makuu kwa Kuimarisha Bandari,Jiji la Ujiji[Ujiji City] Usafiri wa maji na Reli, viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya ziwani,pamoja na masoko ya Biashara za Kimataifa.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Ngome ya Kina mama wa chama hicho Mkoa wa Kigoma Stella Shirima amesema wanaamini Mgombea wao Zitto ataaminiwa na wananchi kwa mara nyingine kutokana na uzoefu wake kisiasa na umahiri wake wa Kujenga hoja Bungeni.
“Siyo kwamba Zitto anahitajika kwetu tu wana Kigoma Mjini naomba niwaambie hakuna muda mwingine wowote muhimu tofauti na sasa ambao Taifa linahitaji watu wa aina hii ya Zitto,nawaombeni msifanye makosa siku ya Uchaguzi”, amesema Stella.
Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria Mkutano huo akiwemo Hamis Juma Abdul mkazi wa Mtaa wa Bushabani Kata ya Kibirizi amesema hotuba ya mgombea ni yenye kujali mahitaji ya wana Kigoma na Taifa kwa ujumla na kwamba endapo ataaminiwa na wananchi anaweza kuwa msaada katika masuala mbalimbali ya Maendeleo ya Taifa.
Social Plugin