Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mgombea urais wa Chama cha Democratic Party (DP), Abdul Juma Mluya, leo Agosti 13, 2025, amechukua rasmi fomu ya kugombea urais katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma,huku akisisitiza dhamira yake ya kuondoa ada za kuhifadhi maiti, akieleza kuwa gharama hizo zinabeba mzigo usiofaa kwa familia ambazo tayari zimewalipa kodi.
“Hakuna sababu ya familia kulia mara mbili au kuathirika kifedha wakati wa msiba,” amesema Mluya.
Mbali na hilo, Mluya amesisitiza marekebisho makubwa ya mfumo wa kikokotoo cha mafao ya wastaafu akieleza kuwa mfumo wa sasa umekuwa chanzo cha kero na dhuluma kwa watumishi waliolitumikia taifa kwa uaminifu.
Amesema Kikokotoo kipya kitahakikisha wastaafu wanapata haki zao kikamilifu, kuondoa umaskini, na kujenga misingi imara ya ajira bora.
Aidha, marekebisho hayo yataenda sambamba na mpango wa waajiri kuwapatia wafanyakazi nyumba bora, kupunguza rushwa na kuongeza ari ya kazi.
Mgombea huyo pia alieleza kipaumbele chake cha askari magereza, akisema hali ya sasa ni ngumu kuwatofautisha na wafungwa kutokana na changamoto za kimaisha na mazingira duni ya kazi.
“Tutaboresha maslahi, mafunzo na mazingira ya kazi ya askari magereza ili kurejesha heshima, nidhamu na weledi wa kitaaluma,” alisema.
Akizungumzia ustawi wa watoto na familia, Mluya aliahidi kutoa bima ya afya ya bure kwa watoto wachanga kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kuzaliwa, pamoja na kuboresha huduma kwa mama wajawazito ili kulinda afya ya mama na mtoto.
Vipaumbele vingine vilivyotajwa ni kukuza kilimo endelevu kwa kuondoa jembe la mkono, kuongeza pato la taifa, na kuboresha mishahara ya askari polisi ili kupunguza rushwa na kuimarisha nidhamu katika vyombo vya ulinzi na usalama.
Mluya alisisitiza kuwa utekelezaji wa vipengele vyake vyote utahakikisha haki, ustawi na maendeleo kwa wananchi wote, ikiwemo wastaafu, askari magereza, mama wajawazito, watoto wachanga, na wakulima.




Social Plugin