
Na Mwandishi Wetu – Malunde 1 Blog
Mkazi wa Mtaa wa Budushi, Kata ya Mwendakulima wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Fatuma Salum (41), Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Busalala, ameuawa usiku wa kuamkia leo kwa kuchomwa shingoni na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana.
Tukio hilo limetokea majira ya saa nane usiku baada ya watu hao kuvunja mlango wa nyumba yake na kutekeleza mauaji hayo, hali iliyozua hofu na taharuki kwa wakazi wa mtaa huo.
Baadhi ya mashuhuda waliozungumza na Malunde 1 blog wakiwemo majirani wamesema marehemu hakuwa na ugomvi na mtu yeyote na kwamba mauaji hayo yamewashitua wakazi wa eneo hilo.
Balozi wa mtaa huo, Philemoni Nyanda, amesema tukio hilo ni la tatu kwa mwaka huu la watu kuuawa kwa kupigwa mapanga au kuchomwa visu katika eneo hilo.
Ametoa wito kwa wakazi kushirikiana na sungusungu na vyombo vya ulinzi ili kuwabaini wahusika.
“Haiwezekani watu waendelee kuuawa na kuishia kusemwa ni watu wasiojulikana. Tukishirikiana na jeshi la jadi tutawabaini. Huyu Mwalimu hakuwa na ugomvi na mtu yeyote, lakini amefanyiwa ukatili wa kinyama,” amesema Nyanda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema kuwa kwa sasa mume wa marehemu (jina linahifadhiwa) anashikiliwa kwa mahojiano.
Amesema upelelezi wa awali umeonesha kulikuwa na mgogoro wa kifamilia.
Social Plugin