Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BAADA YA KUTOSWA CCM, CHIBAGO AIBUKIA CHAUMMA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Mwanga Chibago, aliyekuwa akiwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Mvumi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), sasa ameibuka upya kwa kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA).

Chibago amechukua hatua hiyo baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa awali wa uteuzi ndani ya CCM, ambapo Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho ilimuidhinisha Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ kuwa mgombea wa chama hicho katika Jimbo hilo.

Leo, Agosti 25, 2025, Chibago amekabidhiwa rasmi fomu ya uteuzi na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mvumi, Prudence Kahaya, katika ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) zilizopo Chamwino.

Hatua ya Chibago ni sehemu ya mchakato unaoendelea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ambapo INEC imetoa dirisha la kuchukua fomu kuanzia Agosti 14 hadi 27.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Chibago amesema: “Ninakuja na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi wa Mvumi kwa kuhakikisha wanapata maendeleo ya kweli—barabara zinazopitika mwaka mzima na huduma ya maji safi na salama ni miongoni mwa vipaumbele vyangu.”

Kwa hatua hiyo, Chibago sasa anajiunga rasmi na kinyang’anyiro cha Ubunge kupitia upinzani, akitazamia kuwapa wananchi wa Mvumi chaguo mbadala katika uchaguzi unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com