
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mwanamke aitwaye Pendo Samson Methuthela (37) mkazi wa Kata ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga kwa tuhuma za mauaji ya mpenzi wake, Timotheo Magesa (49), fundi magari mkazi wa Masekelo, aliyefariki dunia baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali (viwembe) kwenye mkono na tumboni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi amesema tukio hilo lilitokea Agosti 23 majira ya saa tatu na nusu usiku katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Bashwee Lodge iliyopo Kata ya Ndala, Manispaa ya Shinyanga.
Kwa mujibu wa Kamanda Magomi, kabla ya tukio hilo marehemu Timotheo alipokea simu kutoka kwa mwanamke asiyefahamika aliyemueleza Pendo aachane naye.
Baada ya mazungumzo hayo, Timotheo alimshawishi Pendo wakaonane katika lodge hiyo, ambapo mzozo ulizuka baada ya Pendo kutaka kufahamu utambulisho wa mwanamke aliyezungumza naye kwa simu akimtaka aachane naye.
"Mwanaume ambaye sasa ni marehemu aliyetambulika kwa jina la Timotheo Magesa, fundi magari mkazi wa Masekelo alijeruhiwa kwa kukatwa na viwembe sehemu za mkono wa kushoto na tumboni na mwanamke aliyejulikana kwa jina la Pendo Samson Methuthela ambaye alikuwa mpenzi wake",amesema Kamanda Magomi.
"Kabla ya Timotheo kukutana na Pendo, mwanamke asiyefahamika alitumia simu ya Timotheo kuongea na Pendo na kumwambia achana na mpenzi wangu, hakupendi. Sasa baada ya hapo Timotheo akamwelekeza Pendo kwamba achana na huyu mwanamke anayesema niachane na wewe. Mimi nakupenda twende tukaonane Bashwee lodge, walipofika hapo Lodge ndipo ugomvi ukaanza, kutokana na Pendo kutaka kumjua huyo mwanamke aliyeongea naye alikuwa ni nani, akashikwa na hasira akamkata kata na viwembe . Kutokana na majeraha hayo akapelekwa hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya matibabu, akafariki dunia saa 6.30 usiku Agosti 24,2025",ameeleza Kamanda.
Aidha, Kamanda huyo amelaani tukio hilo akisema: "Ukatili siyo jambo linalowakumba wanawake pekee, hata huyu mwanaume kafanyiwa ukatili. Ni vyema jamii ikajifunza kuwa na nidhamu na moyo wa kusamehe katika masuala ya mahusiano badala ya kuchukua sheria mkononi, tusiwe na hasira kupita kiasi, tumrudie Mwenyezi Mungu. Huyu Pendo kajichukulia sheria mkononi. Kumchana chana huyu mwanaume na viwembe ni tukio la kusikitisha sana".
Mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.
Social Plugin