Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KALENDA YA UCHAGUZI MKUU YAWEKWA WAZI : INEC YAJIPANGA KWA UCHAGUZI WA KIHISTORIA


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025. Pamoja naye ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani.

Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imezindua Kalenda ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025, huku ikiweka wazi tarehe muhimu na miongozo ya maandalizi kuelekea uchaguzi huo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele amesema kalenda hiyo inalenga kuweka uwazi na kurahisisha ushiriki wa wadau wote wa uchaguzi kwa wakati.

Kwa mujibu wa kalenda hiyo:uteuzi wa wagombea wa Urais utafanyika Agosti 27, 2025, baada ya uchukuaji wa fomu kati ya Agosti 9 hadi 27.

Kwa upande wa Ubunge na Udiwani, uchukuaji wa fomu utaanza Agosti 14 hadi 27, na uteuzi kufanyika tarehe hiyo hiyo ya Agosti 27.

Kampeni za uchaguzi zitaanza rasmi Agosti 28, 2025 na kufikia kilele Oktoba 28, siku moja kabla ya kupiga kura.

INEC imebainisha kuwa jumla ya wapiga kura waliothibitishwa ni 37,655,559 wakiwemo wanawake 18,943,455 na wanaume 18,712,104. Idadi hiyo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 26 ikilinganishwa na uchaguzi uliopita wa mwaka 2020.

Katika hatua nyingine, Tume hiyo imesema vituo vya kupigia kura vimeongezeka kutoka 81,567 mwaka 2020 hadi kufikia 99,911 kwa mwaka huu. Kati ya hivyo, 97,349 viko Tanzania Bara na 2,562 Zanzibar.

Jaji Mwambegele amebainisha kuwa zaidi ya watu milioni 7 wamesajiliwa upya kama wapiga kura wapya, huku wengine zaidi ya milioni 4 wakiboresha taarifa zao.

 Watu waliopoteza sifa au walioandikishwa zaidi ya mara moja wameondolewa au kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Kwa upande wa Zanzibar, wapiga kura 725,876 waliokidhi vigezo vya kisheria vya ZEC watahusika katika kupiga kura ya Rais wa Jamhuri ya Muungano na Wabunge, huku 278,751 waliokosa sifa NEC ikiwaorodhesha kwa matumizi ya upande wa Muungano pekee.


Katika kuelekea uchaguzi huo, INEC imetoa wito kwa vyombo vya habari, asasi za kiraia, viongozi wa dini na wazazi kuhakikisha wanatoa elimu ya uraia, kueleza umuhimu wa kushiriki uchaguzi na kuhakikisha wananchi wanajitokeza kwa wingi kupiga kura.

“Tume itahakikisha haki, uwazi, usawa na ufanisi katika kila hatua ya uchaguzi huu. Huu ni uchaguzi wa kihistoria chini ya sheria mpya – tuushiriki kwa amani,” amesema Jaji Mwambegele.

Kwa mara ya kwanza, uchaguzi huu unatarajiwa kutumia mifumo ya kisasa zaidi ya usimamizi wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na mifumo ya TEHAMA katika mchakato wa kupiga kura na kuwasilisha matokeo.
Sehemu ya viongozi kutoka vyama mbalimbali vya siasa vilivyohudhuria hafla ya uzinduzi wa uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025. 
Sehemu ya viongozi kutoka vyama mbalimbali vya siasa vilivyohudhuria hafla ya uzinduzi wa uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com