
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Chama cha United Democratic Party (UDP) kimeendelea kuwasihi wanachama wake kote nchini kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kabla ya muda wa uchukuaji wa fomu kumalizika tarehe 30 Julai 2025.
Zoezi hilo lilizinduliwa rasmi tarehe 5 Julai 2025, na linaendelea katika ofisi zote za chama kuanzia ngazi ya kata hadi taifa, ambapo fomu za kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinapatikana Makao Makuu ya chama jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa UDP, Saum H. Rashid, nafasi zinazopatikana katika mchakato huu ni pamoja na udiwani (ikiwa ni kwa viti vya kawaida na viti maalum), ubunge (viti vya kawaida na maalum), uwakilishi, urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, urais wa Zanzibar pamoja na nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Katibu Mkuu huyo amesema chama kina dhamira ya kupata wagombea mahiri, wenye sifa, maono na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya kupitia sera mbadala zitakazowagusa wananchi moja kwa moja.
Aidha, Bi. Rashid amewaagiza viongozi wa chama ngazi ya mikoa, wilaya na kata kuhakikisha wanatoa maelekezo sahihi na usaidizi wa karibu kwa wanachama wote wenye nia ya kugombea, ili mchakato huu uwe shirikishi, wa wazi na wa heshima.
“Tunawaomba wanachama wote wenye nia ya dhati ya kulitumikia taifa kupitia UDP kujitokeza sasa. Tusisubiri siku za mwisho. Huu ni wakati wa kuonesha dhamira ya kweli ya uongozi,” amesema.
UDP imeeleza kuwa mchakato wa uchukuaji wa fomu ni hatua ya kwanza kuelekea ushindani wa kidemokrasia unaolenga kuijenga Tanzania mpya yenye usawa, haki na maendeleo kwa wote.
Social Plugin