Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MALUNDE APEWA BARAKA NA CCM KUGOMBEA JIMBO JIPYA LA ITWANGI

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imempitisha rasmi Mhandisi Sebastian Pastory Malunde, mzaliwa wa Tinde, kugombea nafasi ya ubunge kupitia Chama hicho katika Jimbo Jipya la Itwangi, mkoani Shinyanga.

Jimbo hilo limezaliwa baada ya kugawanywa kwa Jimbo la Solwa, na sasa limekuwa uwanja mpya wa kisiasa unaovutia makada wenye sifa na rekodi ya uongozi.

Mhandisi Malunde, ambaye ni mtaalamu mwenye Astashahada ya Juu ya Uhandisi wa Meli pamoja na Shahada ya Uzamili katika masuala ya Uwekezaji na Utunzaji wa Fedha, amekuwa gumzo kutokana na mtazamo wake wa maendeleo na dira aliyonayo kwa ajili ya wananchi wa Itwangi.

Katika hatua hiyo ya awali ya mchakato wa ndani ya CCM, Malunde atachuana na wagombea saba wengine waliopitishwa, wakiwemo makada mahiri kama Azza Hilal Hamad, mkazi wa Tinde pia (aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga kwa kipindi cha miaka 10, ambaye naye ameingia rasmi katika kinyang’anyiro hicho.

Wagombea wengine machachari wenye sifa kede kede waliopitishwa na CCM ni: Chrispine Myeke Simon, Fred Romanus Sanga, John Elias Ntalimbo, Christian Misobi Budoya, Hellena Daudi Mbuli na Anna James Ng’wagi

Kazi kubwa sasa iko mbele kwa kila mgombea, huku kura za maoni ndani ya CCM zikisubiriwa kwa hamu kama kielelezo cha demokrasia ndani ya chama hicho.

Wachambuzi wa siasa za mkoa wa Shinyanga wanatazama kwa karibu ushindani kati ya Malunde, ambaye anajivunia taaluma ya kihandisi na uzoefu wa kitaalamu, dhidi ya Azza Hilal, mwanasiasa aliyebobea katika masuala ya jamii na ustawi wa wanawake.

Jimbo la Itwangi linaonekana kuwa na mvuto wa kipekee mwaka huu, kutokana na kuwa jipya na kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura wapya wanaotamani maendeleo ya haraka na uwakilishi makini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com