SERIKALI YAKANUSHA TAARIFA ZA NDEGE YAKE KUSAFIRISHA MIZIGO HARAMU

Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Msemaji wà Serikali kwebye ukumbi wa habari Maelezo jijini Dodoma.
Msemaji wà Serikali Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.


Na Dotto Kwilasa,Dodoma.

Serikali imekanusha taarifa ya Sekta ya Anga nchini kukumbwa na kashfa nzito ya ndege yake ya mizigo aina ya Boeing767-300F kusafirisha mizigo haramu kwa njia haramu ambayo haijafuata taratibu za kiforodha ambayo inasambaa kwenye baadhi ya mitandao na kueleza kuwa ni  za upotoshaji zipuuzwe.

Hayo yameelezwa leo Mei 30,2023 Jijini hapa na Msemaji wa Serikali na  Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa wakati akizungumza na Waandishi wa habari na kueleza kwamba  taarifa hizo ni za upotoshaji na kwamba zinalenga kurudisha nyuma juhudi za Serikali katika kukuza sekta ya anga na usafiri wa anga. 

Kutokana na hayo Msigwa amesema Serikali inawafuatilia waliochapisha taarifa hizo na hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yao.

Msigwa amefafanua kuwa dege ya mizigo aina ya Boeing767-300F bado haijafika Tanzania, haijaanza kazi rasmi, bado ipo mikononi mwa watengenezaji nchini Marekani. Ndege hii inatarajiwa kupokelewa nchini tarehe 03 Juni, 2023.

"Mheshimiwa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameandaa ndege kubwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner ambayo itabeba wachezaji, viongozi na mashabiki kwenda Algeria kwa ajili ya kuishangilia timu ya Yanga wakati wa mchezo wa pili wa fainali ya Kombe la Shirikisho,"amesema 

Katika hatua nyingine Serikali imewatoa  hofu Watanzania kuhusu  muda wa kuanza kwa majaribio ya treni ya abiria kwa kipande Cha kwanza Cha reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar Es Salaam hadi Morogoro na kueleza kuwa haijadanganya bali kilichotokea ni mabadiliko ya ratiba ya mtengenezaji yalioathiri kuja kwa vichwa hivi.

Imesema kutokuanza kwa majaribio ya treni ya abiria kwa kipande cha kwanza cha reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambayo imeshakamilika, kumesababishwa na kutokukamilika kwa wakati kwa utengenezaji wa vichwa vya treni viwili na mabehewa 30.

Akieleza hayo Mkurugenzi wa Idara hiyo  ya Habari -MAELEZO amesisitiza kuwa sababu ya kutokukamilika kwa vichwa hivyo ni kutokana na changamoto katika upatikanaji wa baadhi ya vipuri.

Msigwa amesema,"Vipuri vinavyotumika kwenye ukamilishaji wa vichwa vya treni ambavyo vinatoka nchini Canada ambako kutokana na changamoto ya UVIKO-19, vita na kuharibika kwa uchumi katika nchi nyingi duniani vimefanya viwanda vingi vinavyozalisha vipuri kutorudi katika ratiba za uzalishaji za kawaida,"amefafanua na kuongeza;

Vipuri tulivyotarajia vitafungwa kwenye vichwa viwili ni miongoni mwa vipuri ambavyo vimepata madhara kutokana na changamoto hizo hivyo, mtengenezaji hakuweza kuleta kwa muda aliopangiwa,"anasema Msigwa 

Pamoja na hayo amesema treni hiyo imeshindwa kuanza majaribio kwa sababu  vichwa vya kuvuta mabehewa havijafika na kwamba Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu ukamilishaji wa vichwa hivyo ili vitakapofika kazi ya majaribio ianzie mara moja.

"Kwa makubaliano mapya tuliyoingia na mtengenezaji wa vichwa vya treni, ameahidi kichwa cha kwanza kitafika mwezi Julai na kikifika tu kitaanza majaribio mwezi huo huo. Kichwa cha pili kitafuata baada ya hapo,"amesema

Amesema Kwa upande wa mabehewa, baadhi yake yameshakamilika na kati ya tarehe 2-3, Juni, 2023 huku kukiwa na matarajia kupokea mabehewa sita ya ghorofa kwa ajili ya kutumika kwenye SGR.

Amesema Mabehewa hayo yamefanyiwa ukarabati na kurejeshwa katika upya wake kwa zaidi ya asilimia 85, haya ni mabehewa ambayo yametoka Ujerumani ambapo jumla yake ni 30. Mabehewa 24 yataendelea kuja kwa awamu.

"Kazi ya ukamilishaji wa mabehewa yanayoendelea kutengenezwa nchini Korea ambayo tayari mabehewa 14 mapya yalishafika na mengine 45 kazi inaendelea kukamilishwa,tunatarajia mabehewa yaliyobaki yatafika nchini wakati wowote ndani ya mwaka huu,mabehewa mengine ambayo tumenunua kutoka China, tunatarajia yatafika mwakani,"amesema 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم