WIZARA YA AFYA YAWATOA HOFU WANANCHI MAAMBUKIZI MAPYA YA MARBURG





Na. WAF - Ziara Mkoani Kagera, Bukoba.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amefanya ziara ya kutembelea katika Kijiji cha Ntoma Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera kwa lengo la kujionea hali inavyoendelea baada ya kutangazwa kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg Mkoani humo. 

Katika Ziara hiyo, Waziri Ummy ameambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Zabron Yoti pamoja na Mwakilishi wa Shirika la UNICEF Bi. Shalini Bahuguna.

Aidha, Waziri Ummy amesema kwa sasa hali ni salama na kuwataka Wananchi wa kijiji hicho na watanzania kwa ujumla kuondoa hofu kwa kuwa Serikali inawajali Wananchi wake. 

“Niwatoe hofu Watanzania tuendelee kufanya kazi zetu lakini tuzingatie maelekezo ya Serikali ya kujikinga na ugonjwa huu kwa kuepuka kushikana mikono hususan kipindi hiki lakini pia tujitahidi kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni.” amesema Waziri Ummy

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na juhudi za kuhakikisha ugonjwa huo unamalizika na hautatokea tena katika maeneo hayo. 

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kanyangele Bw. Hamim Hassan ameishukuru Serikali kwa kufanya juhudi kubwa ambapo hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeongezeka kwa kuthibitika kuwa na ugonjwa huo. 

“Hatua za Serikali kupitia Wizara ya Afya zilizochukuliwa za kuwaweka sehemu maalumu waliokuwa karibu na wagonjwa imesaidia sana kutoendeleza maambukizi kwingine na hali ni shwari kwa sasa.” amesema Bw. Hassan

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments