FALSAFA YA MONTESSORI YATUMIKA KUWANOA WALIMU KAGERA


Baadhi ya Walimu kazini waliohitimu kozi maalumu ya mafunzo mbinu yaliyofanyika kwa miezi sita katika Chuo cha Partage Montessori cha Bukoba
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Yohana Sima akitoa hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila wakati wa mahafali ya mafunzo mbinu kwa walimu ishirini wa shule za msingi Mkoani Kagera yaliyoendeshwa kwa miezi sita katika Chuo cha Partage Montessori.
Baadhi ya wahitimu wa kozi ya miezi sita kwa walimu kazini kupitia Chuo cha Ualimu Partage Montessori wakipokea vyeti wakati wa mahafali ambayo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Yohana Sima kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila
Mkurugenzi wa Shirika la Partage Philippe Krynen(kulia) na Mkuu wa Chuo cha Ualimu cha Partage Montessori cha Bukoba Mkoani Kagera Jacqueline Mwombeki, wakifuatilia matukio wakati wa mahafali ya mafunzo mbinu ya Walimu kazini awamu ya kwanza.
Baadhi ya watoto wanaosoma katika shule ya awali ya Partage ambapo mafunzo yake hufanyika kwa vitendo zaidi kwa kutumia mbinu za Mwanafalsafa Maria Montessori
Mdhibiti Ubora wa Shule kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Agusta Lupokela akitoa salamu wakati wa mahafali ya wahitimu ishirini kutoka shule za msingi za Serikali Mkoani Kagera yaliyoendeshwa kwa miezi sita katika Chuo cha Ualimu cha Partage Montessori Bukoba.

Na Mwandishi wetu

Walimu ishirini walio kazini kutoka shule za msingi za Serikali Mkoani Kagera wamenolewa kutumia Falsafa ya Maria Montessori ambayo watoto wadogo hufundishwa zaidi kwa vitendo huku wakijengwa Kisaikolojia ili wapende kujifunza.


Akifunga mafunzo hayo ya miezi sita yaliyoendeshwa na Chuo cha Ualimu cha Partage Montessori cha mjini Bukoba, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila,amewataka wahitimu kutumia mbinu walizopata kuwasaidia wanafunzi kubadili tabia ili kujenga jamii bora.


Mkuu huyo wa Mkoa ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba,Erasto Yohana Sima,alisema wanatakiwa kuonesha matokeo chanya huku wakitumia lugha rafiki kwa wanafunzi,na kutaka ufuatiliaji uwe unafanyika.


"Elimu mliyoipata isaidie kutatua changamoto za kielimu likiwemo suala la malezi ya watoto wadogo katika jamii yetu,tumieni lugha rafiki na ifikapo mwaka 2025 Halmashauri zitatoa walimu wengi zaidi wa kunufaika na mafunzo haya",alisema Sima.


Naye Mdhibiti Ubora kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Agusta Lupokela alisema Serikali kwa kushirikiana na Wadau wengine wataendelea kusimamia elimu inayotolewa katika ngazi zote na kuwa Shirika la Partage limefanikiwa kutekeleza makubaliano ya mradi.


Aliwaasa wahitimu kujenga taswira njema na kuwa msaada kwa wengine ambao hawajanufaika na mafunzo hayo na kuwa suala hilo linatakiwa kuwa endelevu huku akipongeza Mkoa wa Kagera kwa kuhakikisha hatua hiyo inafanikiwa.


Mkuu wa Chuo cha Ualimu Partage Montessori, Jacqueline Mwombeki,alisema mafunzo mbinu ya Walimu kazini yanajenga hamasa kwa watoto na kuwafanya waongeze bidii katika masomo yao ili waweze kufikia ndoto zao.

Alisema walimu watabadili tabia za watoto bila kutumia nguvu ikiwa ni pamoja na kutowapa adhhabu kali huku wakitumia mbinu walizojifunza kurekebisha tabia za watoto kwa kutumia lugha rafiki itakayowavuta wapende kujifunza.


Maria Montessori ni Mwanafalsafa wa Kitaliano aliyezaliwa mwaka 1870. Alianzisha mbinu za kuwafundisha watoto kwa vitendo zaidi na alitumia muda wake mwingi kutoa elimu kwa watoto waliotoka kwenye familia zenye kipato duni.


Katika risala yao wahitimu hao waliomba Serikali iboreshe miundombinu ya vyumba vya madarasa hasa kuaznia awali hadi darasa la tatu ili waweze kuutumia zana wezeshi watakazopewa kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuwa na kabati imara za kutunzi zana hizo.


Pia walisema idadi ya walimu waliopata mafunzo hayo ni ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa mahitaji,huku wakihaidi kuonyesha matokeo chanya baada ya mafunzo kwamba pia wamefundishwa kutambua mahitaji ya kundi hilo kwa kuzingatia umri wao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments