VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUWAHIMIZA WAUMINI KUHESHIMU IMANI ZA WENGINE

Na Mwandishi wetu,Dar Es Salaam.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amesema ni jukumu la viongozi wa dini kuwaunganisha Watanzania, kudumisha amani, umoja na mshikamano.

Pia, ametaka Viongozi hao kuendeleza utamaduni wa kuheshimu imani ya kila mmoja kwa kutazama mambo mazuri na sio changamoto chache zinazojitokeza.

Kinana ameyasema hayo leo Machi 26, 2023 wakati akizungumza katika hafla ya mashindano ya kuhifadhi na kusoma Kuraani tukufu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Aswhabu al-Kahfi Islamic Centre, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

“Hivi sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameweka mkazo kwenye maridhiano na tuna taasisi ya maridhiano na amani mbayo imeunganisha dini na madhehebu mbalimbali nchini, lengo ni kudumisha umoja, mshikamano na amani katika taifa letu.

“Mimi ningependa kuwasihi viongozi wa dini, kila madhehebu, kila dini ni muhimu tushikame,msitafute mapungufu ya kila mmoja, mtafute mema ya kila mmoja ili tuweze kushikamana,” amesema.

Kinana pia amewasihi  Watanzania kuzingatia na kutanguliza mambo mazuri ya kila mmoja Ili kuondoa uwezekano wa kuibua migogoro isiyo na tija kwa ustawi wa taifa.

Awali akimkaribisha Kinana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo, amesema amani na maadili yanasisitizwa mahali popoote kwani hata Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 imetaja ajenda ya amani na maadili.

"Kila mtanzania ana nafasi ya kukemea tabia zisizofaa kwenye jamii,tuishi Kwa kuzingatia miiko yetu na hii itasaidia kuishi kwenye hali ya utulivu na amani,"amesisitiza Waziri Jafo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments