RPC TARIME : MFANYAKAZI WA BARRICK NORTH MARA ALIKUFA KWA KUJIRUSHA SHIMONI

Kamanda wa Polisi Mkoa Tarime Rorya, ACP Geofrey Sarakikya

***
Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) Tarime Rorya, ACP Geofrey Sarakikya amesema mfanyakazi wa mgodi wa Barrick North Mara, Emmanuel Chacha (26) hakufa kwa kupigwa risasi.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo asubuhi, Kamanda Sarakikya ametupilia mbali taarifa zilizosambazwa kwenye mitando ya kijamii zikidai kwamba mfanyakazi huyo aliuawa kwa kupigwa risasi.

"Maelezo ya watu waliokuwepo kwenye eneo la tukio,na kutokana na matokeo ya uchunguzi wa mwili wa marehemu Emmanuel Chacha  uliofanywa na Daktari katika Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza kifo chake kimetokana na majeraha yaliyotokana na kujirusha kwenye shimo lenye urefu wa mita 20. Taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kifo cha Emmanuel Chacha kilitokana na kupigwa risasi siyo za kweli, huu ndiyo ukweli", amesema Kamanda Sarakikya.


Kamanda huyo wa Polisi ametoa ufafanuzi huo kutimiza ahadi aliyoitoa Machi 12, 2023 kwamba atatoa taarifa kamili ya kifo hicho baada ya kupata majibu ya uchunguzi wa kidaktari kuhusu mwili wa marehemu huyo.


Katika taarifa yake ya awali, kifo hicho kilichotokea Machi 11, 2023 katika eneo la Gokona Underground ndani ya mgodi wa Barrick North Mara, Kamanda Sarakikya alisema kuwa, kabla ya kujirusha kwenye shimo, timu ya kikosi kazi ilimkukuta mfanyakazi huyo akiiba mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu ndani ya mgodi huo.


Alieleza kuwa timu hiyo ya kikosi kazi ilijumuisha afisa madini wa mkoa, maafisa kutoka wa jeshi la Polisi, kitengo cha ulinzi cha mgodi huo na kampuni ya ulinzi ya Nguvu Moja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments