BODI YA BARABARA DODOMA YAPITISHA BAJETI NA MAPENDEKEZO YAKE

 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule.

Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA 
.

SERIKALI kupitia Wakala wa barabara mijini na Vijini (TARURA) mkoani hapa,unatarajia kutumia bilioni 59.86 kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya barabara pamoja na mipango ya matengnezo ya barabara katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Haya yameelezwa leo Machi 16,2023 katika kikao cha  Bodi ya Barabara ya Mkoa ikiwa ni kikao cha pili cha 2022/2023 na Meneja wa TARURA Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe na kuongeza kuwa mapenkezo haya ya mpango wa mwaka 2023/204 yametayarishwa kwa kuzingatia vipaumbele na shabaha ya kuhakikisha  rasilimali fedha zinatumika vizuri kuboresha miundombinu ya barabara.

Mhandisi huyo amesema kuwa mapendekezo hayo yametayarishwa  kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya mwaka wa fedha uliopita 2022/2023 ambapo TARURA ilikua na bajeti ya billion 52.

Amefafanua kuwa mipango ya Jiji la Dodoma katika sekta ya miundombinu hasa barabara inalenga kuboresha barabara zinazolenga kuwepo kwa mzunguko wa magari katika mtandao wa barabara, kuboresha mitaa mikuu ndani ya mji, kusaidia maeneo yote kufikika wakati wote pamoja na kusaidia muunganiko wa huduma za usafiri wa barabara ndani ya Mkoa.

"Jumla ya bilioni 10.86 zinatarajiwa kugharamia kazi mbalimbali za matengenezo ya barabara chini ya wakala wa barabara za mijini na vijijini katika halmashauri zote za mkoa wa Dodoma kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na unatarajia kutumia milioni 834.96 kwa matengenezo katika wilaya ya Bahi, bilioni 1.5 katika wilaya ya Chamwino, milioni 685.6 katika wilaya ya Chemba, bilioni 4.2 katika Wialaya ya Chamwino DC, milioni 682.4 katika Wilaya ya Mji, milioni 863.9 katika Wilaya ya Kondoa DC, BILIONI 1.3 katika Wilaya ya Kongwa na milioni 865.5 katika wilaya ya Mpwapwa” amesema.

Pamoja na hayo amesema kuwa jumla ya bilioni 20.8 zimependekezwa kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ya barabara katika halmashauri za jiji la Dodoma ili kuyawezesha maeneo mbalimbali kufikika wakati wote kwa lengo la kuzisaidia halmashauri kufanikisha mipango mingine na kuhakikisha ujenzi.


“Serikali inataka kuona wananchi wake wanaoishi kwenye miundombinu ya kisasa hivyo mwaka wa fedha 2023/2024 tunatarajia miradi ya maendeleo ya barabara katika Wilaya ya Bahi itagharimu bilioni 4.85, Chamwino bilioni 3, Chemba bilioni 2.7, Dodoma Jiji Bilioni 2, Bilioni 3.3, Kondoa Mji bilioni 3, Kongwa bilioni 5.2 na Mpwapwa Bilioni 5” amesema.


Kilembe pia amesema jumla ya bilioni 13.02 zitokanazo na tozo ya Mafuta zimependekezwa kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ya barabara katika halmashauri zote ili kusaidia muunganiko wa mfumo wa barabara ndani ya halmashauri na mkoa kwa ujumla.

"Katika changanuo huo Wilaya ya Bahi itatumia milioni 950, Chamwino Bilioni 1.9, Dodoma CC Bilioni 4.9, Kondoa Bilioni 1, Kondoa Mjini Bilioni 1, Kongwa milioni 950 na Mpwapwa milioni 950,kutokana na mwenendo wa ongezeko la vyombo vya usafiri jumla ya bilioni 5 kutoka serikali kuu (Jimbo) zimepenekezwa kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ya barabara katika halmashauri kwa mwaka 2023/2024,"amesisitiza 

Kutokana na hayo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani  za pekee kwa Rais Dr. Samia kwa kuendelea kulipa kipaumbele jiji la Dodoma kwa kuongeza bajeti katika sekta ya miundombinu ya barabara huku akitaka ujenzi wa barabara kumalizika mapema na kufikika kirahisi kwa kutoa kipaumbele maeneo ya huduma za kijamii ikiwemo shule, hospitali, sehemu za utalii .

“Bajeti hii imekuwa rahisi sana,nimefurahi tunafanya vizuri na tunaweza kupendekeza bajeti kubwa zaidi kutokana na juhudi za mhe.Rais, tumeona katika kipindi cha miaka miwili bajeji ya TARURA imepanda kwa zaidi ya asilimia 300, tulikua na bajeti ya Bilioni takribani 32 kwa mwaka 2020/2021 lakini mwaka 2022/2023 tuliongezewa mpaka bilioni 52” amesema na kuongeza,;

Niwaombe TARURA na TANROAD hakikisheni  mnaendelea kuongeza ubora na kuweka vipaumbele katika maeneo ya kimkakati pamoja na kuongeza ubunifu ikiwa ni mapendekezo ya bajeti yetu.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments