NEMC KUHAMASISHA UTUNZAJI WA MAZINGIRA KUPITIA SHULE ZA MSINGI, SEKONDARI




Mkurugenzi Mkuu NEMC Dk. Samwel Gwamaka akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma Katika ukumbi wa habari Maelezo.

Mkurugenzi Mkuu NEMC Dk. Samwel Gwamaka akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma Katika ukumbi wa habari Maelezo.



Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA.

Baraza la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)limepanga kuanzisha klabu za utunzaji wa mazingira kuanzia  ngazi ya shule za msingi na sekondari ili kuwajengea watoto  msingi mzuri wa namna ya kutunza na kuhifadhi mazingira katika maeneo yao.

Hayo yamebainishwa Leo March 3,2023 jijini hapa na Mkurugenzi Mkuu NEMC Dk.Samweli Gwamaka wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa baraza hilo  katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita.

Amesema NEMC inaanzisha klabu za mazingira na kuzilea  kwa sababu watoto  wakianza kufundishwa wakiwa katika umri mdogo ni rahisi zaidi kuelewa umuhimu wakutunza mazingira na faida zake kijamii,kiuchumi na kiafya.


“Sasa tunajikita  kuelimisha na kukikamata kizazi cha watoto wadogo kuanzisha shule za msingi na sekondari ili wachukulie suala la utunzaji wa mazingira ni jukumu lao la kila siku katika mwenendo mzima wa maisha yao.Tunaamini watakapo kuwa wakubwa tabia itakuwa imejengeka ,”amesema .

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha usafi wa mazingira  ikiwa ni pamoja na kuhamasisha usafi wa kila jumamosi na  elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ambapo jitihada hizo zimesaidia kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu ambao haujasikika nchini kwa miaka saba mfulululizo ikilinganishwa na miaka  ya nyuma  ikifika kipindi cha mvua lazima wapatikane wagonjwa,”alisema.

Pamoja na hayo Dk.Gwamaka ameeleza kuwa NEMC imeendelea kupokea na kushughulikia malalamiko taklibani 369 ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira kutoka kwa wananchi ikiwemo kuvuja kwa mafuta kutoka kwenye bomba,kuchoma taka hatarishi chini ya kiwango,uchafuzi wa vyanzo vya maji,utiririshaji wa maji taka na uchafuzi wa hewa kutokana na shughuli za viwanda.

Malalamiko mengine wanayoyapokea ni kelele za mziki,kushamiri kwa gereji bubu maeneo ya makazi ya watu,kushamiri kwa vituo vya mafuta katikati ya makazi ya watu,matumizi ya mifuko ya plastiki, na kutoa elimu sahihi na suluhisho kuhusu jambo husika.

“Tumeendelea kufanya ukaguzi katika maeneo taklibani 2133 ya uwekezaji na mazingira yakiwemo maeneo ya mafuta na gesi, matanuru ya kuchomea takahatarishi,maeneo ya machimbo ya makaa yam awe,  pamoja na maeneo ya miradi mikubwa lengo ni kujiridhisha na uzingatiaji wa matakwa ya sheria ya mazingira ya mwaka 2004.

Ameeleza kuwa NEMC imepata mafanikio makubwa ndani ya serikali hii ya awamu ya sita ikiwemo kutokomeza mifuko  ya plastiki ambayo ilikuwa ni kikwazo chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hasaan na Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments