WCF IMELIPA BILIONI 44.6 KWA WANUFAIKA WAKE

 

Na Dotto Kwilasa,DODOMA.

JUMLA ya shilingi bilioni 44.6 zimelipwa na Mfuko wa fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Kwa wanufaika wake kama mafao  ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya kuanza kwa Mfuko huo ambapo malipo ya fidia yalikuwa chini ya sh.milioni 200 kwa mwaka.


Hayo yalibainishwa jijini hapa leo March 2,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dk.John Mduma  wakati akieleza utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita katika ukumbi wa habari Maelezo ikiwa ni mfululizo wa Taasisi za Serikali kueleza shughuli zake.


Amesema hadi kufikia  Juni 30 mwaka jana  WCF imelipa mafao hayo  kwa wanufaika mbalimbali ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri kujisajili katika mfuko huo  hasa katika  kipindi cha awamu ya sita kutokana na hatua za makusudi za kuweka vivutio vya kibiashara na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo na kupunguza viwango vya uchangiaji na kutoa msamaha wa riba.


“Waajiri waliosajiliwa wamegawanyika katika makundi matatu, kundi la kwanza ni la waajiri wakubwa ambao wanachangia kiasi kinachozidi sh.milioni 1.5 kwa mwezi, kundi la pili ni la waajiri wa kati wanaochangia kati ya sh. 250,000 na milioni 1.5 kwa mwezi na kundi la tatu ni la waajiri wanaochangia chini ya sh. 250,000 kwa mwezi,"amesema 


 Dk.Mduma pia amefafanua kuwa mfuko huo ulianza rasmi kukusanya michango kwa waajiri tangu Julai mosi mwaka 2015 ambapo hadi kufikia Juni 30 mwaka jana  makusanyo  yalifikia  sh.bilioni 545.4.


“Katika makusanyo hayo sh.bilioni 88. zilikusanywa mwaka wa fedha 2020/2021 na sh.bilioni 86.6 zilikusanywa mwaka wa fedha 2021/2022.Makusanyo ya michango ya waajiri yalishuka katika mwaka wa fedha 2021/2022 kutokana na kushuka kwa asilimia ya kiwango cha uchangiaji kwa waajiri wa sekta binafsi kutoka asilimia moja  hadi 0.6.


Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa WCF, malipo ya fidia nchini kwa mwaka mzima yalikuwa chini ya sh. milioni 200 lakini baada ya kuanzishwa kwa WCF  malipo yanaongezeka mwaka hadi mwaka. 


Amesema kwa takwimu za mwaka 2016/17, WCF ililipa fidia kwa wanufaika takribani 538 na kiasi cha sh. milioni 613.8  kililipwa huku mwaka 2021/2022 pekee, WCF ililipa fidia kwa wanufaika takribani 1,600 na kiasi cha zaidi ya sh. bilioni 9.33 kililipwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments