WANANCHI TABORA WAISHUKURU SERIKALI UJENZI WA VYUO VYA VETA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Hassan Suluhu akipata maelezo kuhusu ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Hudum cha Mkoa wa Kagera kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Anthony Kasore wakati wa makabidhiano na uzinduzi huo wa Chuo uliofanyika Oktoba 13, 2022.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan Suluhu akiweka jiwe la Msingi Ujenzi wa Chuo cha VETA Mbarali Agasti 8, 2022.

Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Igunga kilichojengwa na Chuo cha VETA Shinyanga.

Jengo la Utawala katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Uyui kiluchojengwa na Chuo cha VETA Tabora.

***************************

*Wadai kuwa Wilaya zimeongeza hadhi kwa kuwa na mafundi wenye ujuzi

Na Chalila Kibuda, Michuzi Tv

Wananchi na wadau mbalimbali mkoani Tabora wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa vyuo vya VETA vya Wilaya ambao umetoa fursa za Wilaya hizo kupaa kimaendeleo.

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inaendelea kukamilisha ujenzi wa vyuo 25 vya Wilaya kwa kutumia nguvu kazi ya ndani yaani force account.

Miongoni mwa vyuo hivyo vinajengwa katika mkoa wa Tabora ambapo Chuo cha VETA cha Wilaya ya Uyui kinajengwa na Chuo cha VETA Tabora pamoja na Chuo cha VETA cha Wilaya ya Igunga kinachojengwa na Chuo cha VETA Shinyanga.

Masele Paulo ni mkazi wa Igunga ambaye amesema kuwa ujenzi wa Chuo cha VETA Igunga umempatia fursa ya kushiriki kwenye kazi ya ujenzi wa chuo hicho kama fundi uashi na kujipatia fedha za kununua viwanja viwili pamoja na kuweza kumsomesha mtoto wake na kuboresha zaidi ujuzi wake.

“Nashukuru sana kutuletea hii VETA…hii VETA imeleta manufaa makubwa kwa wale ambao waliweza kujituma kufanya kazi hapa,” amesema

Mjasiriamali Yunisi Joseph mkazi wa Igunga amesema uwepo wa mradi huo katika eneo lao, umemsaidia kujiongezea kipato na kukidhi mahitaji muhimu kwenye familia yake.

Amesema tangu kuanza kwa mradi huo Aprili 2020, amekuwa akifanya kazi ya kuwapikia wafanyakazi wanaojenga chuo hicho na kwamba kipato alichokipata kimemsaidia kununua kiwanja na kusomesha watoto wake.

“Chuo hiki cha VETA kimetupa faida kweli…mara ya kwanza kabla ya chuo kuanza kujengwa kazi yetu ilikuwa ni kusanya kuni kupeleka kuuza mjini,”amesema Kwa upande wake Emmanuel Rubona mkazi wa Wilaya ya Uyui amesema ushiriki wake kwenye mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA cha Wilaya ya Uyui kama fundi ujenzi kumemwezesha kuboresha ujuzi wake, kumjengea ari na kumwezesha kujiamini zaidi katika kazi.

Mbunge wa Jimbo la Igunga Mhe. Nicholaus Ngassa amesema ujenzi wa chuo cha VETA Igunga umenufaisha wafanyabiashara kutokana na bidhaa za ujenzi kununuliwa wilayani hapo huku jamii ikinufaika kwa mtu mmoja moja kwa kushiriki katika shughuli za ujenzi.

Mhe. Ngassa amewataka vijana kujiandaa vyema kutumia fursa za mafunzo chuoni hapo na hatimaye kuwawezesha kupata fursa za ajira kwenye miradi mbalimbali inayohitaji wataalamu wenye sifa mbalimbali ikiwemo cheti cha VETA.

Amesema kuwa Igunga ni miongoni mwa Wilaya zinazopitiwa na bomba la mafuta kutoka Hoima - Uganda hadi Tanga na kwamba kazi mbalimbali kwenye mradi huo zinahitaji watu wenye ujuzi kwenye fani mbalimbali.

Pamoja na shughuli za ujenzi, VETA pia imetengeneza samani kwa ajili ya vyuo hivyo vipya vya Wilaya kupitia vyuo vyake vyenye fani za Useremala.

Mwalimu wa Useremala katika Chuo cha VETA Tabora Mwesigwa Rwezahula amesema kazi ya kutengeneza samani imesaidia kujiimairisha kwa chuo chake pamoja na wanafunzi na wahitimu wake katika kazi ya utengenezaji wa samani.

Mwanafunzi wa Chuo cha VETA Tabora Agustino Haonga amesema ushiriki wake kwenye mradi wa utengenezaji wa samani umeimarisha uwezo wake wa kufanya kazi kwa vitendo na kumfungulia fursa na matumaini zaidi ya kujiajiri pindi atakapohitimu.

Akizungumzia ujenzi wa vyuo vya VETA, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore amesema VETA inajivunia kukamilisha kwa asilimia 97 ujenzi wa vyuo 25 vya Wilaya kwa kutumia nguvu kazi ya ndani yaani Force Account ambapo mafunzo kwenye vyuo hivyo vipya yanatarajiwa kuanza mwaka 2023 huku vyuo hivyo vikitegemewa kudahili wanafunzi 18,000.

Ametaja vyuo hivyo 25 kuwa ni vya Wilaya za Pangani, Mkinga, Korogwe, Kilindi, Uyui, Igunga, Ikungi, Kishapu, Rufiji, Mafia, Ukerewe, Kwimba, Masasi, Ulanga, Mbarali, Chunya, Butiama, Uvinza, Iringa Vijijini, Buhigwe, Chemba, Bahi, Monduli, Longido na Lushoto.

"Nichukue fursa hii kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini ambayo anaamini ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kiuchumi na kuwezesha vijana kujiajiri "amesema CPA Kasore na kuongeza kuwa Rais Dkt.Samia Hassan Suluhu ameonesha nia yake ya dhati ya kuhakikisha watanzania wanajipatia fursa zaidi za mafunzo ya ufundi stadi ili kuwawezesha kujipatia ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za uchumi.

Kwa mujibu wa CPA. Kasore, Serikali imeshatenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vingine 63 vya wilaya na ujenzi wa chuo cha ufundi stadi na huduma cha Mkoa wa Songwe.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments