WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUACHA UHOLELA MITANDAONI

Msemaji wa Serikali na Idara ya habari- MAELEZO Gerson Msigwa  akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kwenye uzinduzi wa TOMA.


Na Dotto Kwilasa,Malunde1 Blog,DODOMA

MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari-MAELEZO Gerson Msigwa amezindua Taasisi ya Waandishi wa habari mtandaoni (TOMA)huku akiwataka waandishi wa habari hizo kufanya kazi kwa kufuata misingi ya uandishi ili kuondokana na uholela .

Msigwa ameyasema hayo Februari 10,2023 Jijini Dodoma wakati akizindua Taasisi hiyo (TOMA)na kueleza kuwa uholela wa uandishi wa habari unadumaza taaluma hiyo na kusababisha kutoaminika na jamii hivyo kuwataka wanahabari mtandaoni kuzingatia weledi na kutokubali kutumika.

"Zingatieni weledi kuondokana na uholela holela uliopo miongoni mwenu,andikeni kwa kufuata kanuni na kataeni kutumika kwani mkifanya hivyo mtapoteza dhana ya uwepo na ukuaji wa sekta hii,"amesema

Amesema kutokana na kukua kwa matumizi ya TEHAMA,mitandao ya kijamii imerahisisha habari kufika kwa urahisi na kuwa chanzo kikuu cha habari hivyo kuwataka Waandishi wa habari kutumia kigezo hicho kukua kiuchumi na kijamii kwa kuzingatia maadili ya mtanzania. 

"Tasnia ya habari mtandao ipo mikononi mwa vyombo vya habari Mtandaoni, kwa sasa vyombo vya habari Mtandaoni ni  nguzo kubwa kwa sekta ya habari nchini,nitoe tu angalizo kwa sababu kadri zinavyoongezeka inaonekana kama weledi wake unapungua,

Niwatake TOMA kuhakikisha waandishi wa habari mtandaoni wanakuwa na uelewa mkubwa juu ya maudhui wanayoandikà wasiharibu utu wa mtu wala kukiuka haki za binadamu, kinachosumbua Media house nyingi ni weledi, kumeibuka watu ambao wanazusha tu habari zao bila kuzingatia maudhui uandishi hauko hivyo,"amesema

Kutokana na hayo Msigwa amewataka wamiliki wa vyombo vya habari hivyo  kuzingatia weledi katika utendaji kazi wao hasa katika kipindi hiki cha Mapinduzi ya teknolojia kwa kuhakikisha wanazingatia maudhui yanayoendana na taaluma hiyo.

"Sisi tujitahidi kujitofautisha na hao ili tulinde taaluma yetu na Serikali sio kwamba haioni juhudi za vyombo vya habari inaona na ndio maana imetoa uhuru wa kutosha kila mmoja kuanzisha na kumiliki chombo cha habari ila changamoto inatokea namna gani ya kuchuja kipi kiende hewani na kipi kisiende kulingana na maudhui yake,"amesema Msigwa 

Aidha, uzinduzi huo wa TOMA umeratibiwa na Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Arusha (APC) na kuhudhuriwa na wanahabari kutoka mikoa mbalimbali nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments