TCRA YAVIPONGEZA VYOMBO VYA HABARI HAMASA KAMPENI YA KUHAKIKI NAMBA ZA SIMU…..LAINI ZISIZO HAKIKIWA KUFUNGWA FEBRUARI 13


Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa imevishukuru vituo vya utangazaji  (Runinga/Televisheni Redio na Mitandao ya Kijamii ‘Online Tv na Blogs’) kwa ushirikiano vinavyoutoa ikiwemo kuhamasisha wananchi kuhakiki namba za simu.


Akizungumza na Malunde 1 blog, Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo amesema vyombo vya habari vinaendelea kushirikiana vizuri na mamlaka hiyo Kampeni ya kuhakiki Namba za Simu.

Meneja huyo wa TCRA Kanda ya Ziwa amesema Kampeni ya kuhakiki Namba za Simu inamtaka kila mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu, anatakiwa kuhakiki namba yake iliyosajiliwa kwa namba ya Kitambulisho cha Taifa(NIDA).

Mhandisi Mihayo amesema Kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta (EPOCA) 2010, ni kosa kisheria kutumia laini ya simu ambayo haijahakikiwa hivyo kila mwananchi anatakiwa kuhakiki laini yake iliyosajiliwa kwa namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) ili kuepuka kufungiwa laini yake.


“Ili kuhakiki namba yako bonyeza/bofya *106#, chagua namba 5 kisha namba 1 kuhakiki namba kuu. Kama una namba zaidi ya moja, rudia tena zoezi hili kwa kubofya/kubonyeza *106#, chagua namba 5 kisha chagua namba 2 kuhakiki namba za ziada. Kupata maelezo zaidi ya kuhakiki namba yako/zako; tafadhali, tembelea duka au wakala wa Mtoa Huduma wako. Kumbuka Laini zote ambazo zitakuwa hazijahakikiwa baada ya Februari 13, 2023 saa 10 jioni zitafungwa”,amesema Mihayo.


“Ewe mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu, iwapo unapata changamoto kuhakiki namba yako ya simu kwa sababu ulisajili namba hiyo kwa Kitambulisho cha Taifa cha mtu mwingine, tembelea ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), upate namba tambulishi yaani National Idenfitification Number (NIN) itakayokuwezesha kukamilisha usajili wako”,ameeleza.


 MASWALI NA MAJIBU MUHIMU

Zipi ni hatua za kufuatwa ili kuhakiki laini zangu za simu zilizosajiliwa kwa namba ya Kitambulisho cha Uraia?


JIBU: Ili kuhakiki namba zako zilizosajiliwa kwa namba ya Kitambulisho cha Uraia, fanya kama ifuatavyo: -


KWENYE SIMU YAKO:

Bofya *106#(kisha bonyeza kitufe cha kupiga simu kwa mtandao husika;

Menyu itajitokeza kwenye skrini ya kifaa chako cha mawasiliano ikiwa na vipengele vitano (5); 

KUMBUKA: Menyu hii inafanana kwa mitandao yote; 


Ikiwa una namba moja pekee kwa Mtandao husika, unashauriwa kuhakiki kama namba yako ya Kitambulisho cha Uraia ilitumika kusajili namba hiyo pekee, au namba nyingine usizozitambua;

 

Kutekeleza zoezi hili chagua kipengele cha Tatu (3) kwenye menyu inayoonekana kwenye skrini ya kifaa chako. Iwapo utabaini uwepo wa namba za simu usizozitambua fika kwenye duka la Mtoa Huduma wako, ili uzifute.

“Hakikisha unacho kitambulisho chako cha Uraia au NAMBA TAMBULISHI (NIN) ili kukamilisha zoezi hili”

Ikiwa unamiliki namba zaidi ya moja za Mtandao mmoja zilizosajiliwa kwa namba za kitambulisho chako cha Uraia, unapaswa kuzihakiki; 

Kutekeleza zoezi hili, chagua kipengele cha Tano (5) kwenye menyu iliyotokeza kwenye skrini ya kifaa chako. Kisha, bofya kipengele namba (1) ili kuchagua Namba Kuu. halafu, rudia kwa kubofya kipengele namba (2) kuhakiki namba za ziada. 


Ipi ni tarehe ya ukomo ya zoezi la Uhakiki wa Laini za Simu?


JIBU: 

Awali Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) iliweka tarehe-ukomo ya zoezi hili kuwa Januari 31 mwaka huu. Kwa kuona Umuhimu wa kuhakikisha kila Mwananchi anaetumia huduma za Mawasiliano hakosi huduma hizo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye (Mb.) alitangaza wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari Dodoma mnamo tarehe 24 Januari 2023 kuongeza muda wa zoezi hili kutoka tarehe ya awali Januari 31 hadi Februari 13, 2023 saa 10:00 jioni.


Mara baada ya tarehe ukomo kupita laini za simu ambazo hazitakuwa zimehakikiwa kwa kufuata utaratibu uliobainishwa zitazuiliwa KUTOA na KUPOKEA huduma/zitafungwa. 


Zipi ni faida na hasara za kutohakiki laini zangu za simu?


JIBU: Faida za kuhakiki laini zako zilizosajiliwa kwa Kitambulisho cha Uraia ni nyingi, kama ifuatavyo: -


Uhakiki unakuhakikishia Usalama wako wewe kama mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu;

Ni utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) na Kanuni zake zinazoelekeza kwamba laini zote zisajiliwe kwa utaratibu bayana;


Zoezi hili litawezesha kuondoa kwenye ikolojia ya Mawasiliano simu-laghai zinazosababisha matukio ya uhalifu miongoni mwa watumiaji wengine wa huduma za Mawasiliano ya simu;

Uhakiki unakupa utambulisho thabiti (Digital identity). Unakuwezesha wewe Mwananchi kuwa mshiriki Madhubuti katika Ujenzi wa uchumi wa Taifa lako (Uchumi wa Kidijitali). 

Kuboresha Huduma. Taarifa za watumiaji zilizokamilika zinaiwezesha Serikali kupitia TCRA kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za Mawasiliano. 


Hasara za kutohakiki ni kama ifuatavyo:-

Utakosa huduma. Laini yako itafungwa.

Kuunganishwa kwenye jinai.


Vipi ikiwa nilimsajilia mtu mwingine Laini ya Simu? 


JIBU: 

Ikiwa ulimsajilia mtu mwingine laini ya simu, mtake akasajili laini yake kwa utambulisho wake mwenyewe, kwa kufuata utaratibu uliobainishwa; ikiwa ni pamoja na kupata namba ya kitambulisho cha uraia kutoka NIDA.


Wewe uliemsajilia unalazimika/ unapaswa kuwasiliana na mtoa Huduma ili afute usajili wa namba ya huyo uliemsajilia na kuhamisha usajili kwa kutumia utaratibu uliowekwa. 


Izingatiwe kwamba:     Kila mtumiaji wa Mawasiliano ya simu nchini, aliekidhi vigezo vya kuwa na kitambulisho wa uraia anapaswa kwa mujibu wa kanuni za usajili wa laini za simu, kusajili na kuhakiki laini zake kwa utambulisho wake husika.


Mnasema zoezi hili litapunguza Uhalifu, kivipi?


JIBU: 

Ni sahihi kwamba zoezi hili litapunguza matukio ya utapeli mtandaoni kwa kuwa, itakuwa rahisi sasa kumtambua kila mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu. Utambulisho halisi wa kila mtumiaji sasa utakuwa umetunzwa vema katika Kanzidata.

 

Kwa sasa baadhi ya watumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu wenye nia ya kutenda uovu kwenye Mtandao wamekuwa wakijificha kwenye kichaka cha usajili wa watu wengine kwa kutenda makosa ya kimtandao kwa kuwa usajili wa laini za simu wanazotumia si wa kwao; 


Hivyo, tukihakiki wote na kuondoa namba tusizozitambua na kuhakikisha wale tuliowasajilia wao pia wanasajili laini zao wao wenyewe tutafanikiwa kupunguza matukio ya utapeli mtandaoni kwani kila mtumiaji atatambuliwa kwa laini yake ya simu anayotumia.


Ilikuwaje watu wakawa na laini za simu zisizokuwa na utambulisho wao?

Baadhi ya mawakala wa watoa huduma hawakuwa waaminifu, walikuwa wakiwasajilisha wenye vitambulisho zaidi mara moja na kutengeneza laini za simu za ziada, tofauti na ile ya muhusika kisha kuziuza laini hizo, ambazo wenye nia mbaya wamekuwa wakizitumia kutenda makosa ya kimtandao; 


Mawakala hawa wasio waaminifu TCRA tuliwadhibiti kwa kushirikiana na Watoa Huduma, na tukatoa maelekezo kwa Watoa Huduma kuhakikisha mawakala wao wanazingatia sheria na taratibu zilizopo wanaposajili laini za watumiaji wapya au wale wanaohitaji kuongeza laini za simu;


Nikufahamishe kwamba tumeendelea kuzifutia huduma laini hizi za simu zinazotenda makosa mtandaoni ambapo hadi Novemba mwaka jana 2022 tulifungia laini zaidi ya 52,000 zikiwemo zilizokuwa zikijihusisha na utapeli. 


Baada ya tarehe ya mwisho kupita 13/02/2023 ndiyo itakuwa basi tena?

JIBU:  Zoezi hili ni endelevu. Hata hivyo kwa wale wenye laini zinazotumika sasa, ikiwa hawatakuwa wametekeleza takwa la uhakiki tutaziondolea huduma itakapofika tarehe ya ukomo, ili kuhakikisha kila mtumiaji wa huduma za Mawasiliano, anatambuliwa na kumbukumbu yake inatunzwa kwenye Kanzidata, hii itawezesha Serikali yetu kuwa na takwimu sahihi na kamili za watumiaji halisi wa huduma za Mawasiliano ya simu, intaneti na huduma za kifedha mtandaoni. 


Ikiwa nitabaini uwepo wa namba za simu nisizozitambua baada ya kutekeleza zoezi la Uhakiki, nifanyeje?

JIBU:   Fika kwenye duka la Mtoa Huduma wako, kisha toa Taarifa ya namba hizo ili ziweze kufutwa kwa kuzingatia utaratibu wa bayometria na kuwasilisha namba za Kitambulisho chako cha uraia. 


Je, mnafikiria kuongeza Muda zaidi?

Tayari muda umeongezwa kutoka tarehe-ukomo ya wali ambayo ilikuwa Januari 31, 2023 na sasa zoezi la uhakiki wa laini za simu zinazotumika limeongezewa muda hadi Februari 13, 2023.


Zoezi hili la kuhamasisha uhakiki wa laini za simu zinazotumika lilianza Desemba 2021.


Mnataka kufunga hilo zoezi mbona wananchi hatujapata Taarifa za kutosha?

Kampeni hii ya Elimu tunaiendesha kwa ushirikiano na watoa huduma wote wa huduma za Mawasiliano ya simu. Kwa upande wao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii, pia wamekuwa wakituma ujumbe wa moja kwa moja kwa watumiaji wote wa Mawasiliano ya simu wakiwakumbusha kila mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu kuhakiki laini zao za simu. Hivyo, TCRA tunaamini kila mtumiaji wa Mawasiliano ya simu amepokea Taarifa hizi za uhakiki kupitia ujumbe mfupi uliotumwa na watoa huduma, au kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya TCRA, watoa huduma na Wizara ya sekta. 


Zoezi linaendaje hadi sasa?

  Zoezi linaendelea kwa mafanikio makubwa. Hadi sasa zaidi ya asilimia 90 ya laini za simu zinazotumika nchini zimehakikiwa. Hivyo hima! mtumiaji wa huduma za Mawasiliano wewe ambae bado hujakamilisha uhakiki wa laini zao za simu, tekeleza zoezi hilo sasa kwa kubofya *106# kisha fuata maelekezo.


 Muhimu kukumbuka ni kwamba itakapofika tarehe 13 Februari 2023 kama laini yako haijahakikiwa itazuiliwa kutoa na kupokea huduma. Hakiki sasa!


***

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments