WAENDESHA BODABODA WACHAFUKWA UJENZI BARABARA YA LUBAGA KUCHUKUA MUDA MREFU..."NJIA YA MCHEPUKO HATARI...TUNATOZWA FAINI KIHUNI"

Vifusi vikiwa barabarani

Na Halima Khoya - Malunde 1 blog
Waendesha pikipiki maarufu 'Bodaboda' katika Manispaa ya Shinyanga wameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya kutoka Shinyanga Mjini kuelekea Old Shinyanga (Lubaga) ili kutokana na kwamba njia ya mchepuko iliyowekwa kwa ajili ya kutumia siyo salama na ni hatari kwa watu na mali zao.


Wakizungumza na Malunde 1 blog wamesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo umetumia muda mrefu tangu Oktoba 2022 hadi sasa hivi mwezi Februari, 2023 na kwamba njia ya mchepuko iliyowekwa kwa ajili ya kutumia siyo salama na ni hatari kwa watu na mali zao.


Waendesha bodaboda hao akiwemo Juma Pius na Hamis Mathayo wamesema matengenezo ya barabara hiyo ni changamoto kwao kwani wanatozwa faini zisizo na ulazima (50,000 hadi 500,000) ambazo ni kinyume na sheria huku akiiomba serikali kumaliza haraka ujenzi huo ili kufanya kazi kwa uhuru.

"Nilikuwa na mteja nimempakia nikawa nimepita barabarani ghafla nikakutana na mkandarasi amesimama mbele yangu ikabidi nikatishe, katika harakati za kujitetea nikakunja pembeni wakati huo katikati ya barabara wamefunga waya kiasi kwamba hata ukienda vibaya unakufa,ikabidi nisimame wakachukua pikipiki wakapeleka kituoni, wakasema faini laki 5 ndipo alikuwepo kiongozi mwingine akasema faini ya ardhi ya TANROADS ni elfu 50,ikabidi nilipe nikapewa risiti ndiyo nikarudishiwa pikipiki yangu", amesema Pius.


Nao wajasiriamali wa vyakula na matunda Lubaga, Magret Samwel na Johan Shilla wamesema kuwa adha wanayokumbana nayo ni kukosa wateja hali inayosababishwa na kizuizi cha kukatisha barabara kwenda upande mwingine ili kutoa huduma zao hali inayorudisha nyumba mzunguko wa biashara zao.


"Mfano nina mteja kando ya barabara inanibidi nizunguke umbali mrefu sana ili nifike alipo hivyo tunakosa wateja wengi, tunaiomba mamlaka husika ifanye haraka kukamlisha ujenzi huu ili tuendelee na biashara zetu zinazotupatia kipato",amesema Shilla.


Kwa upande wake Meneja TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Mibara Ndirimbi  amesema kuwa Mkandarasi aliyechukua kazi hiyo yupo ndani ya muda ambapo mkataba wake ni wa miezi 8 na anatarajia kumaliza ujenzi huo mwezi wa 6 mwaka huu sambamba na kwamba hakuna faini inayotozwa kwa wananchi.


Ndirimbi amesema kuwa baadhi ya malighafi zinazotumika katika ujenzi huo zikiwemo kokoto zinatoka  nje ya Shinyanga ambapo amebainisha kuwa wakandarasi wanaofanya ujenzi huo wametoka ndani ya nchi ya Tanzania hivyo vifaa anavyotumia katika ujenzi huo ni vichache.


"Mkandarasi yupo ndani ya mkataba wa siku 240 ambayo ni miezi 8,hivyo tunaomba muwe wavumilivu, pia wakandarasi waweke tahadhari kwa wananchi pia wakandarasi wawasikilze wananchi bila kugombana", amesema Ndirimbi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments