KIKWETE ATAKA MIPANGO MIJI KUPITIWA UPYA



Na Dotto Kwilasa, Malunde I Blog-DODOMA.


NAIBU Waziri wa Ardhi ,Nyumba na maendeleo ya makazi Ridhiwan Kikwete 
amezielekeza Mamlaka za upangaji, wataalamu wa ardhi na mipango Miji kuona haja ya kupitia upya suala la mpangilio wa ujenzi wa makazi ya Jiji la Dodoma ili kuondoa ongezeko la migogoro ya ardhi na makazi holela. 

Kikwete ameeleza hayo leo Jijini hapa kwenye uzinduzi wa bodi mpya ya wakurugenzi ya usajili wa wataalamu wa mipango Miji na kueleza kuwa kutokana na ujenzi holela kumekuwa na malalamiko mengi ya uvamizi wa ardhi Jijini Dodoma Kutokana ma ujenzi holela usiofuata taratibu na kanuni za mipango Miji.

Amesema ili Jiji liwe la kisasa mipango Miji inapaswa izingatie makazi ya watu na kueleza kuwa hakutakiwi kuwe na sehemu za starehe katika maeneo ya makazi huku akiwaonya wataalamu wa ardhi kutowaruhusu wanasiasa kuwaongoza. 

Amesema ili kuondokana na ujenzi holela ni lazima wananchi  waelimishwe, wajue kwa undani, na wakiri kukerwa na ujenzi au uendelezaji ardhi kiholela na kwamba elimu hiyo itawahamasisha wananchi walioendeleza ardhi kiholela kuchangia gharama za uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi hasa kupitia upangaji shirikishi (urasimishaji).

"Tunayo kazi ya kusimamaia zaidi,Bado masta plani ya Jiji hili haiko sawa kuna baadhi ya viwanja vimepimwa kiwanja  juu ya viwanja natoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kutoa kipaumbele kuhusu utoaji elimu ya upangaji wa matumizi ya ardhi na kuhimiza uandaaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi 
ya ardhi katika miji, miji midogo na vijiji,"amesema.  
 
Amesema ushirikishaji wa wadau wote katika upangaji wa Ardhi ni suala la msingi ili kuepusha migogoro pamoja na hasara za kiuchumi na kimazingira, ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mipango hiyo. 

"Ushiriki wa wadau wengine wenye maslahi katika ardhi kwa sasa siyo wa kuridhisha sana, jambo linalosababisha maslahi yao kutozingatiwa kikamilifu kwenye mipango ya matumizi inayoandaliwa hili linajidhihirisha kwa kuwepo na migogoro mingi ya mwingiliano wa matumizi ya ardhi mijini na vijijini,"amesema na kuongeza;

Mfano eneo la nzuguni kuna watu walitolewa kwenye maeneo yao huo ni uonevu mkubwa,matokeo yake kuna watu waliotoka Dar ndio wanao milikishwa maeneo hayo kwa kuonekana wao ndio Wenye hadhi ya kuishi nzuguni,"amesema

Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa Migogoro ya aina hiyo hukwamisha shughuli nyingi za maendeleo hivyo, ni muhimu  kuwashirikisha wadau kutoka sekta nyingine za maendeleo wakati wa kuandaa mipango miji ili isikinzane na mipango ya sekta zao.  

Kuhusu kukabiliana na uhaba wa watumishi amesema Bodi kwa kushirikiana na Wizara hiyo, itaendelea kuomba vibali vya uhamisho wa watumishi kuhamia Bodi, kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na kuwajengea uwezo watumishi waliopo.  

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo Prof.John Lupala amesema bodi hiyo itafanya kazi ya kusimamia utekelezaji wa bodi kwa kuzingatia sheria na  kanuni zinazoongoza mipango Miji. 

Amesema kwa kuzingatia uzoefu na weledi walionao katika fani mbalimbali watashirikiana kikamilifu na Wizara kuendeleza taaluma ya Mipangomiji kwa pamoja na kufikia lengo la kusimamia Wataalam wa Mipangomiji na kampuni za upangaji miji. 

Prof.Lupala amesema bodi hiyo itasimamia Wataalam na Kampuni za Mipangomiji kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za upangaji miji, kutoa huduma bora, kuweka mazingira ya kuvutia Wataalam wa Mipangomji waliokidhi vigezo vya kusajiliwa ili wasajiliwe, pia kuzalisha fursa zaidi za ajira na kuongeza mchango katika pato la taifa.

Amesema kwa mujibu wa Sheria, Bodi imepewa dhamana ya kuisimamia taaluma ya Mipangomiji pamoja na Wataalam wa Mipangomiji, hivyo watahakikisha wanaweka mipango kuifanya taaluma ijulikane kwa wananchi na pale ambapo mtaalam au kampuni imefanya kazi kinyume na maadili zichukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.  
 
"Tunaahidi kufanya kazi kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu, kwa maslahi mapana ya nchi yetu na kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo ili kuhakikisha kwamba, Bodi inakidhi matarajio ya wadau na kuleta tija katika utekelezaji wa majukumu lakini jambo kubwa zaidi tutabuni mbinu za namna bora ya kuimarisha utendaji kazi wa Wataalam na Kampuni za Upangaji Miji pamoja na kuibua mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili taaluma hii na Sekta ya Ardhi kwa ujumla,"amesisitiza  
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri ameeleza kuwa ili ardhi ithaminiwe lazima kuwe na uhifadhi ardhi ili miji ipangwe na kuwa na hadhi nzuri.

Aidha ameishauri bodi hiyo kutengeneza na kuandaa mpango kazi wa ardhi ili kuboresha miundombinu ya majiji 
ikiwa ni pamoja na kusajili wataalamu wa ardhi kwa kuhusisha makampuni ya upimaji ardhi kuondoa migogoro ya ardhi.

Mkuu huyo wa Wilaya pia ameishauri elimu kwa Umma ifanyike ili wananchi wajue namna ya kuimiliki ardhi kihalali  na kuondokana na migogoro iliyopo ambayo kwa kiasi fulani inakwamisha shughuli za maendeleo.

"Tuwaelimishe wananchi kuhusu ardhi,nguvu tunayotumia zaidi kubomoa makazi tuielekeze zaidi kwenye elimu kwa Umma hii itasaidia uwepo wa udhibiti wa mpango Miji,"amesema





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments