WAZIRI MABULA AONYA WANAOOMBA VIBALI VYA UJENZI KINYUME NA MIPANGO KABAMBE

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam wakati wa zoezi la utoaji hati tarehe 19 Desemba 2022. Kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Almas Nyangasa.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkamkabidhin hati mkazi wa Kigamboni wakati wa zoezi la utoaji hati tarehe 19 Desemba 2022 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Almas Nyangasa.


Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Fatma Almas Nyangasa akizungumza wakati wa zoezi la utoaji hati lililofanyika wilayani Kigambano tarehe 19 Desemba 2022 jijini Dar es Salaam.Sehemu ya wakazi wa kigamboni waliojitokeza katika zoezo la utoaji hati lililofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula tarehe 19 Desemba 2022. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

………………………

Na Munir Shemweta

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameonya wale wanaoomba vibali vya ujenzi kwa ajili ya ukarabati majengo na badala yake wanafanya ujenzi bila kuzingatia mipango kabambe ya uendelezaji miji katika maeneo husika kuacha mara moja

Waziri Dkt Mabula ametoa onyo hilo leo wilayani Kigamboni mkoa wa Dar es Salaam wakati wa zoezi la utoaji hati kwa wananchi wa wilaya hiyo waliorasimishiwa makazi yao akiwa katika ziara yake ya siku nne mkoani Dar es Salaam.

Akitolea mfano wa mkoa wa mwanza na Kigamboni, Dkt Mabula amesema baadhi ya wananchi wameomba vibali kwa ajili ya ukarabati wa majengo na badala yake usiku wanabomoa jengo zima na kujenga usiku na mchana nyumba za kawaida ama maduka jambo ambalo ni kinyume na utaratibu mzina wa mpango kabambe wa uendelezaji miji.

Ametaja maeneo yenye mchezo huo katika mkoa wa Mwanza kuwa ni pamoja na Nyamaga, Pamba na Mabatini ambapo alisisitiza waliopewa vibali na kwenda kinyume na utaratibu wa mipango ya uendelezaji miji kusimamisha ujenzi mara moja kwa sababau ni lazima wajenge kwa mujibu wa mpango kabambe wa halmashauri husika.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza wakurugenzi na makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa kuhakikisha wanapita na kukagua kama kuna vibali vipya vilivyotolewa na ujenzi kufanyika kinyume na mipango kabambe ya uendelezaji miji kusitishwa mara moja.

“Tunahitaji kutengeneza miji yetu hatuhitaji kurudi nyuma, gharama iliyotumika kwenye uandaaji master plan ni kubwa sana, sasa haiwezekani kujengwa nyumba mpya katika eneo lenye mastaer plan” alisema Dkt Mabula

Sambamba na onyo hilo Dkt Mabula pia ameagiza makampuni manne yaliyokuwa yakifanya kazi ya urasimishaji makazi nchini kutopewa kazi kwenye halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam na nje ya mkoa huo mpaka hapo Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji itakapojiridhisha na adhabu ilihotolewa kwa kampuni hizo kutokana na mapungufu mablimbali yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji miradi ya urasimishaji makazi holela na kuyataja makampuni hayo kuwa ni Hosea co. ltd, Makazi Consult Ltd, Visible Planners na Ereco Development Estate Ltd

‘’Tunataka tutoe fundisho maana kazi ya urasimishaji imekuwa na kelele sana na lawama hizo zomeelekezwa au kuishia wizara ya ardhi wakati maelekezo ya mhe Rais katika kutekeleza zoezi la urasimishaji ni kushirikisha makampuni binafsi kwa lengo la kuleta ufanisi’’ alisema Dkt Mabula.

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametaka wananchi wanaovamia maeneo ya ardhi kuchukuliwa kama wamefanya kosa la jinai na siyo wavamizi wa kawaida. Dkt Mabula alisema kumekuwa na tabia inayoonesha kuwa wananchi wanaochukua ardhi za watu kama wavamizi wakati watu hao wanatenda kosa la jinai na kusisitiza kuwa watu hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua kama wakosaji wengine wa jinai.

Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Fatma Almas Nyangasa alimuambia Waziri wa Ardhi kuwa wilaya yake inaendelea kujipanga vizuri katika masuala ya ardhi na kufanikiwa kuhakikisha maeneo yanapangwa na kupimwa kwa maelekezo ya mipango miji ingawa inakabiliwa na changamoto za vitendo vya uvamizi vinavyofanywa na baadhi ya watu wasio waadilifu na kubainisha kuwa tatizo hilo wanaendelea kupambana nalo.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam Shukran Kyado alisema kuwa, ofisi yake imekuwa ikishirikiana vyema na halmashauri ya Manispaa ya kigamboni katika masuala ya ardhi na kubainisha kuwa kuanzia julai 2022 idara ya ardhi kwenye halmashauri hiyo imefanikiwa kuandaa jumla ya hati 4,722.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments