TAKUKURU YAZINDUA PROGRAMU RAFIKI KUSAIDIA JAMII KUKATAA RUSHWA.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama.

Mkurugenzi  wa TAKUKURU CP. Salum Hamduni.

Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 Blog DODOMA. 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imefanya Mkutano wake  Mkuu wa Mwaka unaoenda sambamba na uzinduzi wa Programu ya TAKUKURU rafiki Kwa  lengo la kutoa elimu kwa wananchi juu ya rushwa.

Aidha Mkutano huo uliowashirikisha watendaji wa TAKUKURU wa mikoa, Wilaya na vituo maalumu utatumika kutathmini utendaji kazi wa Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuona namna ya maboresho ya kupiga hatua katika kuondoa rushwa na viashiria vyake.
 
Akizungumza leo Novemba 19,2022 kwenye mkutano huo Jijini hapa, Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama ameitaka Taasisi hiyo nchini (TAKUKURU) kuona namna ya kuwashirikisha Viongozi wa dini Katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.

Waziri huyo ameongeza kuwa Kwa kuwashirikisha Viongozi hao jamii itafahamu madhara ya rushwa na kuwa na utayari wa kukemea vitendo hivyo kwa kuwa jukumu la kuzuia rushwa na viashiria vyake ni la kila mtanzania.

 Sambamba na hayo ametaka TAKUKURU kutumia mkutano huo kufanya vipimo vya rushwa kwa kila mkoa na kuvitangaza ili jamii ifahamu namna inavyopaswa kuwajibika katika mapambano hayo .

Amesema mikoa  itakayoonekana ina kiwango kikubwa cha rushwa itapaswa  kujitafakari na kuja na majibu kwenye mkutano kama huo mwakani 2023.

Amesema kuwa lengo la tathmini hiyo ni kupimana na kuona ni mkoa upi ambao unakiwango kikubwa cha rushwa na upi unakiwango kidogo cha rushwa kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia watendaji kujitadhimini katika maeneo yao.

Amesema,"Mapambano yenu mnayapeleka zaidi katika kupambana na rushwa lakini haiwakatazi na haiwaondoi kwenye majukumu yenu ya kila siku kwani  majukumu mliyopewa ni ya kushughulika na kupambana na rushwa ujenzi wa maadili na stahiki kwa watumishi wa umma;

"Nyie makamanda wangu wa Mikoa mahali pa kuanza ni kwa huyo Katibu Tawala msaidizi anayeshughulikia Utawala na rasilimali watu akiweza huyo kufanya kazi zake vizuri mienendo na vitendo vya unadhulifu wa fedha za taifa hili letu kwenye Halmashauri zitapungua ama kuisha kabisaa kutaneni nao hawa,"amesema.

Hata hivyo amefafanua kuwa kuzuia vitendo vya rushwa ni gharama ndogo ikilinganishwa na gharama zinazotumika kwenye mapambano hivyo kuitaka Taasisi hiyo kuongeza nguvu zaidi katika mapambano kwa kuanza na kuzuia.

Kwa upande wake Mkurugenzi  wa TAKUKURU CP. Salum Hamdun amesema Pamoja na changamoto zilizopo Katika masuala ya rushwa nchini,Tanzania ni moja ya nchi sita duniani zilizotangazwa kupiga hatua katika masuala ya mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini.

Amezitaja nchi nyingine zilizopiga hatua kuwa ni pamoja na Ethiopia,Sisheli,Angola,Rwanda na Senegal ambazo zimepiga hatua kutokana na utafiti uliofanywa na mashirika mbalimbali likiwemo la Transparent International.

Amesema kuwa pamoja na hayo pia Tanzania imepanda nafasi ya 87 kwa mapambano dhidi ya rushwa kati ya nchi 187 ambazo zimefanyiwa utafiti na mashirika mbalimbali.

"Tunashukuru kufikia nafasi hiyo naimani tutaendelea kupanda zaidi nafasi za juu katika mapambano dhidi ya rushwa,"amesema.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa mapambano dhidi ya rushwa niya kila mmoja hivyo kila mtu anapaswa kumuangalia mwenzake anayehusika na vitendo dhidi ya rushwa.

Mkurugenzi huyo pia amezungumzia kuhusiana na uzinduzi wa program Rafiki ya kupambana na rushwa kuwa  itapelekwa kila mahali mpaka kwenye kata ambapo itawasaidia wananchi kujua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao.

Amesema ni jukumu la kila mmoja kupambana na rushwa na si Taasisi hiyo  pekee hivyo wananchi pia  wanapaswa kutoa taarifa ambazo zinaviashiria vya rushwa ili kuzishughulikia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments